Somalia yafungua tena ubalozi Marekani

Somalia
Image caption Somalia ilimteua balozi wake Marekani mapema mwaka huu

Somalia itafungua tena ubalozi wake nchini Marekani leo miaka 25 baada ya ubalozi huo kufungwa.

Mwandishi wa BBC Abdullahi Abdi anasema hii ni hatua kubwa sana kwa Somalia na kwa Wasomali karibu 200,000 wanaoishi Marekani.

Maafisa wa serikali ya Somalia wanasema kufunguliwa kwa ni ishara ya hatua zilizopigwa tangu kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo 1991.

Uhusiano kati ya Somalia na Marekani umekuwa ukiimarika tangu Agosti 2012, Somalia ilipofikisha kikomo kipindi cha mpito na kuteua viongozi wapya.

Rais Obama aliteua balozi wa kwanza wa Marekani Somalia Februari mwaka huu, na miezi miwili baadaye waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry akawa waziri wa kwanza wa kigeni wa Marekani kuzuru Mogadishu.

Somalia nayo iliteua balozi wa kuiwakilisha Marekani.

Licha ya hatua hiyo inayoashiria kuimarika kwa hali Somalia, hali ya usalama bado haijadhibitiwa na mashambulio ya mara kwa mara ya kundi la al-Shabab huripotiwa, hasa Mogadishu.