Wanawake 100 wa BBC 2015: Nani wenye msukumo zaidi?

wanawake
Image caption Msimu wa Wanawake 100 ulianza 2013

Wanawake mia wenye msukumo zaidi duniani mwaka wa 2015 wameorodheshwa na BBC.

Makala ya mwaka huu ya Wanawake 100 ni ya tatu tangu kuanzishwa kwake 2013, na lengo lake ni kuwakilisha wanawake vyema katika habari zinazopeperushwa na BBC

Orodha ya mwaka huu inajumuisha mshindi wa Oscar, Mwigizaji Hillary Swank na mwanamitindo kutoka Sudan Alek Wek.

Orodha hiyo pia inajumuisha wawekezaji 30 wenye umri wa miaka 30 kwenda chini na wanawake wenye msukumo wa ajabu walio na miaka 80 kwenda juu.

‘Kutoogopa hatari’

Makala haya ya BBC ya Wanawake 100 mwaka huu pia yanaangazia wahudumu wa afya wenye ujasiri, watengenezaji filamu ambao wanabuni filamu zinazonakili changamoto na matarajio kwenye jamii zao na pia viongozi katika nyanja za sayansi, siasa, elimu na sanaa

Mmoja wa walioorodheshwa ni mwakamke mmoja kutoka Argentina Estela de Carlotto 84, anayefanya kazi ya kupatanisha watoto na wazazi wao ambao walinyakuliwa wakiwa watoto wakati wa utawala wa kijeshi wa 1970.

Yeye mwenyewe alikutanishwa na mjukuu wake mwaka wa 2014.

Wajasiriamali wetu, ambao ni wachanga kwa vizazi viwili ukiwalinganisha na Carlotto, wanatupatia ushauri wa kuweza kufanikiwa.

Mjasiriamali Mjerumani Antonio Albert mwenye umri wa miaka 25 ni mwanzilishi wa Careship, ambalo huendesha huduma ya mtandaoni ya kuduma ya kuwatunza wazee.

Anawashauri wanawake "wawe wenye ujasiri na wasiogope hatari”.

Orodha yetu imejumuisha pembe zote za dunia kutoka kwa Li Tingting, ambaye ni mwanaharakati wa haki za wanawake wapenzi wa jinsia moja kule Uchina hadi kwa Chimala, Malawi, ambaye ni mkunga. Ina pia mwandishi wa vitabu kutoka Lebanon Jana el-Hassan na mchekeshaji kutoka Marekani Megan Grano.

Ujasiri

Baadhi ya wanawake kwenye orodha yetu wana ujasiri sana, kwa mfano Neyda Rojas kutoka Venezuela, mtawa ambaye hutembelea magereza nchini humo ambayo huwa yamejaa wafungwa kupindukia. Magereza hayo ni moja ya yale hatari zaidi duniani.

Msimu huu utaanza na wiki mbili za vipindi vya kusisimua na makala mtandaoni.

Kule India, miongoni mwa mengine tutaangazia wasichana wanaozaliwa jimbo la mgharibi la Maharashtra, ambao hupewa jina 'nakusha' maana yake ikiwa hawatatikani kwenye jamii. BBC itazungumza na baadhi ya wasichana waliopewa jina hilo miaka minne iliyopita.

Tukielekea Burkina Faso, tunakutana na wanawake walioachwa na mabwana zao waliohamia Ulaya, baadhi kwa miezi kadha na wengine miaka.

Na kule Mashariki ya Kati, tutazungumza na ‘Malala’ wa Syria, Maisoun Almellehan,16, ambaye ni mkimbizi Jordan. Almellehan anajizatiti sana kuhimiza wasichana wakimbizi waende shuleni na kusoma.

Msimu huu wa Wanawake 100 utafikia kilele kwa mjadala kuhusu sura, uongozi na mahusiano katika maeneo 100 mbalimbali kote duniani – ikiwa ni pamoja na Albania, Kosovo, Samoa, Fiji, Israel na Jamaica – na katika makao makuu ya BBC jijini London.

Makala za msimu wa BBC wa Wanawake 100 zitapeperushwa mtandaoni, katika BBC World News TV, na BBC World Service pamoja na idhaa 28 za lugha mbalimbali kuanzia Novemba 18 hadi Desemba 2.

Jiunge na mjadala katika Facebook, Twitter na Instagram, kwa kutumia kitambulisha mada #100Women.