Mkutano mkubwa wa albino wafanyika Dar

Albino
Image caption Changamoto zinazowaathiri watu wenye ulemavu wa ngozi zinajadiliwa mkutanoni

Viongozi wa vyama na mashirika ya watu wenye ulemavu wa ngozi kutoka nchi zaidi ya 30 za Afrika na Ulaya wanakutana kwa siku mbili Dar es Salaam, Tanzania.

Kwa mujibu wa waratibu wa mkutano huo, lengo la kuwakutanisha ni kuwajengea uelewa wa jinsi ya kutetea haki zao.

Mwandishi wa BBC Aboubakar Famau aliyeko Dar es Salaam anasema hii ni mara ya kwanza kwa mkutano wa aina hii kufanyika.

Image caption Washiriki wanatarajiwa kufahamiana na kubadilishana mawazo

Ingawa lengo la mkutano huo ni kubadilishana mawazo na kuwawezesha kufahamiana, Vicky Ntetema ambaye ni mkurugenzi wa shirika la Under the Same Sun anasema ana matumaini makubwa sana kuhusu mkutano huo kwamba mengine mengi yatawezekana.

“Tunategemea wakitoka hapa watakuwa wamejifunza mengi. Mfano kutumia vyombo vya habari kuelimisha jamii kuhusu ulemavu wa ngozi na jinsi ya kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi ambao hhupata madhira makubwa sana na kubaguliwa katika nchi zao,” anasema.

Mkutano huu pia, umekusanya watu mbali mbali wakiwemo wataalamu wa jenetikia, uoni hafifu na wataalamu wa ngozi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.

Imeelezwa kwamba, lengo kwa kuwepo kwa wataalamu hawa, ni kuwawezesha watu wenye albinism kuijua hali yao kiafya ili waweze kujitetea vizuri zaidi.

“Maeneo mengi duniani ulemavu huu wa ngozi watu hawauelewi vyema. Wangu wengi hudhani watu hawa ni wa ajabu. Jukumu hili wanapewa viongozi hawa, waweze kujijua vyema zaidi na kutetea haki zao,” anasema Bi Ntetema.

Image caption Washiriki wamekiri kuwepo kwa mwamko mpya kuhusu haki za albino

Baadhi ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo, wanakiri kuwepo kwa mwamko wa kutetea na kulinda haki za watu wenye ulemavu wa ngozi katika miaka ya hivi karibuni, lakini wakati huo huo baadhi wanasema jitihada hizo zimeshindwa kuzaa matunda stahiki kwa sababu ya kukosekana kwa uelewa katika jamii.

Kassim Kazungu kutoka Burundi anasema kutoelewa vyema ulemavu wa ngozi ndiko kumekuwa kukiwafanya watu hawa kubaguliwa katika jamii.

Tofauti na miaka iliyopita, katika nchi nyingi hivi sasa watu wanajitokeza na kutoa taarifa kuhusu ukatili unaoendelea dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Hata hivyo, imeelezwa kwamba, licha ya vitendo vya ukatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kupungua nchini Tanzania, lakini imearifiwa kuwa, vitendo hivyo ikiwemo ukataji wa viungo vimeanza kuongezeka katika nchi jirani ambazo watuhumiwa wake wamekiri kuvipeleka nchini Tanzania.