Moja kwa Moja: Shambulio hotelini Bamako

Bofya hapa kwa habari za karibuni zaidi

Image caption Maafisa wa polisi wakiwasaidia mateka kutoka ndani ya hoteli ya Mali

2016:Washambuliaji walikuwa wakisema ''Allahu Akbar'' walipoingia ndani ya hoteli hiyo huku baadhi ya mateka wakisema kwamba waliwasikia wakionga kiingereza.

20.15:Washambuliaji walitumia magari yenye nambari za usajili za kidiplomasia

20.04:Kufikia sasa idadi ya watu wanaodaiwa kuuawa katika hoteli hiyo ni 18 huku maafisa wawili wa polisi wakijeruhiwa

Image caption Mateka asaidiwa kutoka

19:10 Ubelgiji imesema afisa mmoja wa serikali yake ni miongoni mwa waliouawa kwenye hoteli ya Radisson, Mali. Geoffrey Dieudonne alikuwa Mali kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa serikali.

19:08 Waziri wa usalama wa Mali Salif Traore aambia kikao cha wanahabari kwamba watu wenye silaha walioshambulia hoteli ya Radisson kwa sasa hawazuilii mateka wowote. Afisi ya Rais imeandika kwenye Twitter ikishukuru maafisa wa usalama na mataifa yaliyosaidia kukabiliana na shambulio hoteli hiyo ya kifahari.

18:10 Shirika la Reuters linasema kundi la wapiganaji wa kijihadi la al-Murabitoun limedai kuhusika kwenye shambulio hoteli ya Radisson Blu mjini Bamako. Tangazo hilo limefanywa kupitia akaunti ya Twitter ya kundi hilo, ingawa habari hizo haziwezi zikathibitishwa. Kundi la Al-Murabitoun linajumuisha makundi mawili ambayo yalijitenga kutoka kwa tawi moja la al-Qaeda eneo la Afrika Kaskazini.

18:00 Waziri wa mashauri ya kigeni wa Algeria amesema raia saba wa Algeria ni miongoni mwa watu waliookolewa Bamako, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Image caption Vikosi vya kijeshi ndani ya Hoteli ya Radisson

17:13 Wizara ya usalama Mali imetangaza kwamba wapiganaji watatu kati ya walioshambulia hoteli ya Radisson, Bamako wameuawa, tovuti ya Abamako inaripoti.

17:00 Wanajeshi maalum wa Marekani wanasaidia katika operesheni hoteli iliyovamiwa Bamako, kituo cha runinga cha CNN charipoti.

16:17 Maafisa wa ubalozi wa India nchini Mali wameambia BBC kuwa raa wa India waliokuwa kwenye hoteli ya Radisson Blu wako salama.

Awali, ripoti zilikuwa zimesema kulikuwa na Wahindi 20 waliokuwa wakiishi katika hoteli hiyo.

"Tumewasiliana nao. Kuna raia 200 wa India nchini Mali," ubalozi huo umesema.

16:10 Runinga ya taifa ya Uchina imeripoti kuwa raia wanne wa Uchina waliokuwa wamekwama hoteli ya Radisson Blu "wameokolewa".

Awali runinga ya CCTV ilikuwa imeripoti kuwa raia 10 wa Uchina walikuwa wameshikiliwa mateka.

15:55 Waziri wa masuala ya ndani wa Mali Meja Kanali Salif Traoré amewaambia wanahabari nje ya hoteli ya Radisson Blu kwamba watu watatu wameuawa na wanajeshi wawili kujeruhiwa kwenye operesheni inayoendelea hotelini humo. Watu 30 waliokuwa wameshikiliwa mateka ndani ya hoteli hiyo pia wameokolewa na maafisa wa usalama.

15:40 Polisi wa Ufaransa wamepakia kwenye Twitter picha za polisi maalum wakielekea Bamako kutoka Paris.

15:20 Kikosi cha polisi 50 maalum kutoka Paris kimetumwa kwenda Bamako ambako hoteli ya Radisson ilishambuliwa asubuhi, shirika la AP limeripoti.

15:08 Kituo cha taifa cha runinga Mali kinaripoti kuwa mateka 80 wameokolewa kutoka hoteli ya Radisson Blu. Awali, wamiliki wa hoteli hiyo walikuwa wamesema watu 170 walikuwa wanazuiliwa mateka.

Haki miliki ya picha AFP

14:50 Shirika la Reuters linasema wanajeshi maalum wa Mali wameingia hoteli ya Radisson iliyoshambuliwa na watu wenye silaha mapema leo.

Haki miliki ya picha AFP

14:40 Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius amehutubia wanahabari na kusema Ufaransa itachukua "hatua zifaazo" kukabili watu walioshambulia hoteli Bamako. Amesema kikosi cha dharura kimewekwa kulinda ubalozi wake Bamako.

14: 25 Shirika la habari la Reuters limemnukuu afisa mmoja wa serikali ya Uturuki akisema wafanyakazi watatu wa shirika la ndege la Uturuki wamefanikiwa kutoka kwenye hoteli iliyoshambuliwa Bamako.

14:00 Mwanamuziki mashuhuri kutoka Guinea Sekouba Bambino ni miongoni mwa waliofanikiwa kutoka kwenye hoteli iliyoshambuliwa. Ameambia wanahabari: "Niliamka na kusikia milio ya risasi, nilidhani walikuwa wezi tu waliokuwa wakitaka kuiba. Baada ya dakika 20 au 30 hivi, niligundua hawakuwa wezi wa kawaida."

13:55 Mwafrika tajiri zaidi Aliko Dangote kutoka Nigeria amesema hakuwepo kwenye hoteli iliyoshambuliwa Bamako. Anasema alikuwa nchini Mali jana.

Haki miliki ya picha AFP

13:50 Shirika la habari la AFP linaripoti kuwa wanajeshi sasa wanaingia hoteli ya Radisson Blu mjini Bamako.

13:35 Ikulu ya Rais yasema Rais Ibrahim Boubacar Keïta ambaye amekuwa mjini N'Djaména, Chad kwa mkutano wa mataifa ya Sahel atarejea Bamako katika saa chache zijazo kufuatia shambulio hotelini Bamako.

13:30 Mmoja wa maafisa wa usalama ameambia Reuters kuwa washambuliaji walisikika wakiimba "Allahu Akbar" walipokuwa wakiingia hoteli ya Radisson Blu. Allahu Akbar ni Kiarabu maana yake Mungu ni Mkubwa.

13:29 Ikulu ya Rais wa Mali imesema watu 170 wameshikiliwa mateka kwenye hoteli hiyo ya Radisson Blu.

13:20 Shirika la habari la Reuters linasema wapiganaji wamewaachilia baadhi ya wateka, wakiwemo wale walioweza kukariri Koran. Shirika la AFP nalo linasema maafisa wa usalama wa Mali wameonekana wakisindikiza wanawake wawili kutoka upande wa hoteli hiyo.

13:15 Kituo cha redio cha kibinafsi cha RTL kinachotangaza kutoka Paris kimesema wanajeshi wa Ufaransa pia wametumwa katika hoteli hiyo. Wanajeshi hao wamekuwa Mali tangu Januari 2013 wakisaidia jeshi la Mali kupambana na wapiganaji wa kiislamu kaskazini mwa nchi hiyo.

13:14 Wanajeshi wamewasili katika nje ya hoteli hiyo kwa mujibu wa shirika la habari la AFP ambalo pia limepiga picha hizi.

Haki miliki ya picha AFP
Haki miliki ya picha AFP

12:58 Shirika la habari la Reuters linasema walinzi wawili wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo hoteli Radisson Blu wakinukuu mkuu wa walinzi hao. Kampuni inayomiliki hoteli hiyo inasema watu wawili wenye silaha wanawazuilia watu 170 - wageni 140 na wafanyakazi 30.

12:55 Shirika la habari la Uchina la Xinhua linasema kuna Wachina kadha ambao wamekwama katika hoteli ya Radisson Blu mjini Bamako, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

Haki miliki ya picha Radisson Blu Hotel
Image caption Hoteli hiyo yenye vyumba 190 inamilikiwa na Wamarekani

12:51 Tovuti ya habari ya Depeche Du Mali nchini Mali imeripoti kuwa watu kumi ndio walioshambulia hoteli hiyo ya Radisson Blu.

12:50 Kampuni ya Rezidor Hotel Group inayomiliki hoteli hiyo imesema juhudi zinafanywa kudhibiti hali na kuongeza kwamba kulikuwa na wageni 140 hotelini ambao wamezuiliwa na "watu wawili".

12:42 Ubalozi wa Marekani Bamako umeandika kwenye Twitter ukiwataka wafanyakazi wake kukaa maeneo salama, nao raia wakiweza, wawasiliane na jamaa zao.

12:30 Watu wenye silaha wameshambulia hoteli ya Radisson Blu katika mji mkuu wa Mali, Bamako, ripoti zinasema

Haki miliki ya picha Radisson Blu Hotel