Wabelgiji watakiwa waondoke Burundi

Burundi
Image caption Chama tawala kimedai Ubelgiji inawaunga mkono wapinzani

Chama tawala nchini Burundi kimewataka raia wote wa Ubelgiji waondoke nchini humo.

Hatua hiyo inajiri wiki moja baada ya Ubelgiji kuwataka raia wake walio nchini muhimu kwa shughuli ambazo “si muhimu sana” waondoke kutokana na ongezeko la machafuko.

Burundi imeituhumu Ubelgiji kwa kuwa na uhusiano na makundi ya kigaidi ambayo inalaumu kwa kuongezeka kwa visa vya mauaji.

Ubelgiji ilisema ina raia karibu 500 nchini Burundi lakini mwandishi wa BBC Robert Misigaro anasema bado hakuna dalili za raia hao kuondoka.

Anasema taarifa hiyo ya chama tawala cha CNDD-FDD itazidisha uhasama kati ya mataifa hayo mawili.

Taarifa ya CNDD-FDD ilisema tahadhari iliyotolewa na Ubelgiji majuzi kwa raia wake inaonyesha “wanasiasa wakoloni wa Ubelgiji wako tayari kufanya lolote lile kuhusiana na masuala Burundi.

Watu 240 wameuawa kwenye machafuko nchini Burundi tangu Aprili na miili ya watu waliouawa katika njia isiyoeleweka imekuwa ikipatikana mara kwa mara barabarani.