Papa Francis kuzuru Afrika mara ya kwanza

Papa Francis
Image caption Papa Francis atatembelea Msikiti mjini Bangui

Papa Francis anatarajiwa kuanza ziara yake ya kwanza kabisa barani Afrika Jumatano Novemba 25.

Kwenye ziara hiyo ya siku sita itakayomfikisha Kenya, Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Papa anatarajiwa kueneza ujumbe wake wa Amani, maridhiano, mashauriano na kuchochea juhudi za kuzima migawanyiko.

Mataifa yote matatu yamekuwa yakijiandaa kumkaribisha kiongozi huo wa Kanisa Katoliki duniani, na msisimko mkubwa unashuhudiwa kote.

Afisa wa mawasiliano wa Vatican Padri Federico Lombardi alisema Alhamisi kwamba kwa Jorge Mario Bergoglio, ambalo ndilo jina kamili la Papa Francis, hii itakuwa ziara yake ya kwanza kabisa Afrika.

Itakuwa ziara ya 11 ya Francis akiwa kama papa nje ya Vatican. Mapapa wawili wamewahi kuzuru mataifa haya kabla yake.

Wa kwanza alikuwa Papa Paul VI aliyezuru Uganda mwaka 1969. Baadaye Mtakatifu John Paul II alizuru mataifa 42 ya Afrika akitembelea Kenya mwaka 1980, mwaka 1985 na mwaka 1995; Uganda mwaka 1993; na Jamhuri ya Afrika ya Kati 1975.

Kwa mujibu wa Vatican Radio, Papa Francis staandamana na waziri wa mashauri ya kigeni wa Vatican Kadinali Pietro Parolin, na naibu wake Angelo Becciu.

Ataandamana pia na Kadinali Filoni anayesimamia Kongamano la Kueneza Injili pamoja na Kadinali Turkson anayeongoza Baraza la Amani na Haki la Kanisa Katoliki.

Atatembea pia na wafawidhi wa sherehe, wafanyakazi mbalimbali wa Vatican, wanahabari 75 na maafisa wa usalama.

Wakati wa ziara yake Papa Francis anatarajiwa kusherehekea misa na waumini, kukutana na viongozi wa kisiasa na kidini, kubadilishana mawazo na maaskofu, kutangamana na maskini na pia kukutana na vijana.

Nchini Kenya pia atahutubia viongozi na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, nchini Uganda asherehekee wafia dini wa Uganda, na nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati afungue kanisa kuu la Holy Door mjini Bangui.

Mjini Bangui pia, kabla ya kukamilisha ziara yake, atatembelea Msikiti wa Kati na kukutana na Waislamu huko.

Jamhuri ya Afrika ya Kati imetatizwa sana na makabiliano kati ya Wakristo na Waislamu.