Mapadri waliojitoa Kanisa Katoliki kwa sababu ya useja

Huwezi kusikiliza tena

Miongoni mwa mambo ambayo waumini wa Kanisa Katoliki wanatarajia Papa Francis azungumzie ni upungufu wa makasisi Kanisani.

Wachache miongoni mwa wanaokubali wito wa kuwa padri, wanajikuta katika ushawishi mkubwa wa kukiuka amri ya kuishi maisha ya useja hivi kwamba wanaondoka Kanisani au kujikuta katika kashfa za kuzini na kuliharibia Kanisa jina.

Mwandishi wa BBC Muliro Telewa alitembelea Magharibi mwa Kenya, ambako aliongea na baadhi ya mapadri waliojitenga na Kanisa Katoliki na kuamua kuoa.

Mapadri hawa sasa hufuata kanisa la Reformed Catholic Church of Kenya, ambalo ni tawi la Ecumenical Catholic Church.

Kanisa hilo lilijitenga kutoka Kanisa Kuu Katoliki duniani na kupinga amri ya Kanisa Katoliki kuwa mapadri wao wote wanapaswa kuwa waseja.

Ibada katika kanisa hilo huwa ni ile ile ya Kitatoliki - nyimbo, vitabu sawa, mishumaa sawa hata majoho ya mapadri ni yale yale.

Image caption Padri Akwale na mkewe Gladys

Padri Wilberforce Anyanga Akwale, wa Kanisa la Mtakatifu Antony, Kongoni alifanywa padri mwaka 1995 katika Kanisa Katoliki katika eneo la Mukumu, Magharibi mwa Kenya. Anasema kuwa alikutana na mkewe, Gladys, akiwa mpenzi wake mwaka huo huo alipofanywa padri.

Katika mahuburi aliyotoa baada ya mahojiano na BBC, Padri Akwale alisema alijitenga na Kanisa Katoliki la Kirumi kwa sababu walitaka watu wafahamu kuwa mapadri wa kanisa hilo wanaoa.

“Tulitaka kufanya mambo yetu hadharani watu wajue kuwa mapadri wetu wanaoa. Sio kufanya usherati usiku na kisha unakuja kanisani na kusema; Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Hapana,” anasema.

Padri Akwale anasema kuna mapadri wengi wanaoishi maisha ya usherati au na wengine ndoa za siri.

"Nilifanya kazi ya Mungu lakini sikuwa na talanta ya kukaa bila mke. Bibilia inaniambia Unapoenda kulala na kahaba inamaanisha mko mwili moja na huyo kahaba,” anasema.

"Mimi nikaamua kuachana na maisha hayo mabaya kwa kujiondoa na kujitokeza hadharani.”

Padri Akwale ana mke kwa jina Gladys na watoto watano wenye umri wa kati ya miaka tisa hadi 18.

Wengi wa waumini wa Kanisa la Reformed Catholic Church of Kenya wanaungana na padri wao.

Kuna wale wanaosema kuwa Bibilia inawataka watu duniani waendelee kuzaa na kuujaza ulimwengu.

Kuna wengine wanaosema kuwa kwa kuwa miongoni mwa mambo mengine ya padri ni kutoa ushauri nasaha kwa waumini, na ni vigumu kwa mtu asiye na mke kuwashauri wenzake.

Mapadri walio katika Kanisa Katoliki asilia, yaani Kanisa Katoliki la Kirumi, wanatetea amri ya Kanisa kwa mapadri kuwa waseja maisha yao yote.

Image caption Padri Vincent Shamalla anaamini mapadri wanaotaka kuoa wanafaa kujiondoa kanisani

Padri Vincent Shamalla wa Parokia ya Mtakatifu Marko, katika Jimbo la Kakamenga anasema padri aliyetawazwa kisha akajiingiza katika maisha ya ndoa anafaa kujitangaza na kuondoka katika huduma.

Mbali na swala la useja Papa anatarajiwa pia kushughulikia matatizo ya ndoa za wake wengi, shughuli za ubatizo wa watoto katika familia hizi na hata ndoa za watu wa imani mbalimbali.