Wakaazi milioni 2 wa Crimea hawana umeme

Haki miliki ya picha RIA Novosti
Image caption Crimea haina umeme

Ripoti kutoka Crimea zinasema kuwa jimbo hilo limebakia katika giza baada ya nyaya za umeme kutoka Ukraine kulipuliwa usiku wa kuamkia leo.

Nyaya zote nne zinazopeleka umeme katika jimbo hilo la Crimea zimekatwa sasa na kuwaacha wakaazi zaidi ya milioni mbili bila umeme.

Picha zilizosambazwa kupitia mitandao ya kijamii zinaonesha nyaya za umeme zikiwa zimetundikwa bendera ya Ukraine.

Crimea ilimegwa kutoka Ukraine na Urusi mwaka uliopita lakini utawala nchini Ukraine umekuwa ukipeleka umeme eneo hilo.

Viongozi wa jimbo hilo wanasema kuwa wamejaribu kurejesha umeme katika miji ya Simferopol, Yalta na Saky wakitumia generata lakini hautoshi.

Kwa mujibu wa naibu waziri wa Crimea, Mikhail Sheremet, hospitali na zahanati zingine za afya ndizo zilizopewa kipaombele.

Haki miliki ya picha RIA Novosti
Image caption Crimea ilimegwa kutoka Ukraine na Urusi mwaka uliopita lakini utawala nchini Ukraine umekuwa ukipeleka umeme eneo hilo

Hata hivyo Wizara inayoshughulikia majanga ya kitaifa imetangaza hali ya tahadhari na kuamuru maafisa wake wawe macho wakati huu.

Laini mbili kati ya nne tayari zilikuwa zimekatwa kufuati mlipuko ya siku ya ijumaa

Utawala nchini Ukraine unasema kuwa ulikabiliana na wanaharakati wakati walijaribu kurekebisha laini hizo.