Cameron kukutana na Hollande kujadili IS

Cameron Haki miliki ya picha PA
Image caption Kwa sasa ndege za Uingereza haziruhusiwi kushambulia Syria

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron atakutana na Rais wa Ufaransa Francois Hollande kujadili juhudi za pamoja na kupambana na Islamic State.

Ufaransa inataka kuwe na muungano wenye nguvu zaidi wa kukabiliana na IS.

Mkutano huo huenda ukaongoza juhudi zozote za baadaye za Bw Cameron kujaribu kushawishi bunge la nchi hiyo kuunga mkono mashambulio ya angani Syria.

Mkutano huo unajiri siku chache baada ya kundi la IS kudai kuhusika katika kutekeleza mashambulio Paris ambayo yaliua watu 130.

Kundi hilo pia lilikiri kuhusika katika mashambulio ya majuzi Tunisia, Misri, Beirut na Uturuki.

Ijumaa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa kauli moja azimio la kuongeza mara dufu juhudi za kukabiliana na IS.

Hayo yakijiri, Bw Hollande anatarajiwa kukutana na Rais wa Marekani Barack Obama ikulu ya White House Jumanne, kujadili zaidi juhudi za jamii ya kimataifa kukabiliana na wapiganaji hao.

Baadaye, anatarajiwa kuelekea Urusi kwa mashauriano sawa na Rais wa Urusi Vladimir Putin.