Pfizer yainunua kampuni ya dawa ya Allergan

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Pfizer yainunua kampuni ya dawa ya Allergan

Kampuni inayotengeza dawa ya Viagra inayotibu upungufu wa nguvu za kiume,Pfizer imeungana na kampuni ndogo inayotengeza dawa aina ya Botox inayotumika na wanawake kuficha makunyanzi (wrinkles) Allergan kwa kima cha dola bilioni $160bn.

Kampuni hiyo itakuwa moja ya kampuni kubwa zaidi ya kutengeza madawa duniani.

Wandani wa maswala ya kiuchumi wanasema kuwa muungano wa kampuni hiyo umechochewa pakubwa na kuimarika kwa kiwango cha kodi ya uzalishaji nchini Marekani.

Pfizer inaaminika kuwa inakwepa kodi hiyo ya juu kwa kuhamia mjini Dublin Ireland ambayo ni makao makuu ya Allergan.

Wenye hisa wa kampuni hiyo ya Allergan watatuzwa hisa 11.3 ya muungano wa kampuni hiyo mpya.

Kimsingi,wenye hisa wa Pfizer watapata hisa moja kwa kila moja waliokuwa nayo.

Haki miliki ya picha GETTY
Image caption Allergan hutengeza dawa aina ya Botox inayotumika na wanawake kuficha makunyanzi (wrinkles)

Mwaka uliopita kampuni ya kutengeneza madawa ya Pfizer ilikusudia kununua kampuni ya AstraZeneca yenye makao yake makuu nchini Uingereza hata hivyo mkataba wao ulivunjika pale wenye hisa wa kampuni hiyo ya Uingereza ilipodai Pfizer ilikuwa ikiwadunisha.

Mkataba huu mpya unatarajiwa kukamilika mwakani.

Pfizer inatarajia kuokoa dola bilioni $2bn katika kipindi cha miaka 3 ijayo.

Mkurugenzi wa kampuni ya Pfizer , Ian Read atakuwa mwenyekiti na mkurugenzi mkuu mtendaji wa muungano wa kampuni hiyo huku mwenyekiti wa Allergan Brent Saunders,akipewa wadhfa wa afisa mkuu wa uzalishaji.