Faru walio hatarini wasalia 3 pekee Kenya

Haki miliki ya picha AP
Image caption Faru walio hatarini wasalia 3 pekee Kenya

Mmoja wa faru wanne weupe wenye asili ya kaskazini, ambao ndio waliosalia dunia pekee yao ,amefariki dunia.

Faru huyo mweupe aliaga dunia katika hifadhi moja ya wanyama nchini Marekani.

Hali ya kiafya ya faru huyo wa kike aliyepewa jina Nola, na aliyekuwa na umri wa miaka 41, ilianza kudorora, baada ya kufanyiwa upasuaji majuma mawili yaliyopita.

Afya yake ilizidi kudorora na ndipo aliporuhusiwa kufa, jana Jumapili.

Nola amekuwa kivutio cha wengi katika hifadhi ya wanyama cha San Diego Safari Park, tangu mwaka 1989.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Nola, na aliyekuwa na umri wa miaka 41, ilianza kudorora, baada ya kufanyiwa upasuaji majuma mawili yaliyopita.

Faru watatu weupe waliosalia duniani ni wazee na wanalindwa kwa masaa 24, katika mbunga ya wanyama pori ya Ol Pejeta, nchini Kenya.

Kuna takribani faru 20,000 wenye asili ya kikusini duniani, lakini utafiti bado unaendelea kubainisha iwapo ikiwa chembe chembe za uzazi za faru hao zinaweza kuoana na zile za faru wenye asili ya kikaskazini.

Watafiti wanasema ikiwa mpango huo utafaulu, huenda ndama wa faru mwenye asili ya kikaskazini akazaliwa katika kipindi cha kati ya miaka 10 na 15 ijayo.