Albamu ya Adele kuandikisha historia

Haki miliki ya picha PA
Image caption Adele

Huenda Album ya mwanamuziki maarufu wa Uingereza Adele ikaandikisha historia ya kununuliwa kwa kasi sana kwa muda wa wiki moja, ambapo kwa siku tatu nakala nusu milioni tayari zimeuzwa.

Kufikia sasa nakala 538,000 za Albamu hiyo kwa jina "25" zimenunuliwa, zikiwa zimesalia siku nne kwenye chati ya wiki.

Ni albamu mbili pekee ambazo zimewahi kuuza nakala zaidi ya nusu milioni kwa wiki moja.

Albamu ya "Take That Progress" iliyoandaliwa na bendi ya Uingereza ya "Take That" ilifaulu kuuza nakala 519000 mwaka wa 2010, huku "Oasis's Be Here Now" inayoshikilia rekodi hadi sasa ikiuza nakala 696,000 mwaka wa 1997.

Hayo yakiarifiwa albamu ya Elvis Presley "If I Can Dream" ambayo kwa wakati mmoja iliongoza chati nchini Uingereza ni ya pili kwenye chati za katikati mwa wiki, huku "Purpose" ya Justin Beiber ikishikilia nambari tatu.