Mvulana aliyetuhumiwa kuwa 'gaidi' adai fidia

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ahmed Mohammed Kijana aliyentengeza saa na kutuhumiwa kuwa kilipuzi

Mvulana wa umri wa miaka 14 aliyezoa umaarufu baada ya kukamatwa kwa kupeleka saa ya kujitengenezea shuleni, anadai fidia ya dola milioni 15 ($15m).

Ahmed Mohammed alitiwa mbaroni na polisi wa mji wa Irving, jimbo la Texas nchini Marekani baada ya saa yake kudhaniwa kuwa kilipuzi na baadaye akafukuzwa shule.

Taarifa ya wakili wake inasema tukio hilo lililogonga vichwa vya habari duniani, lilimfanya apokee vitisho na kumsababishia matatizo ya kisaikolojia.

Ahmed na familia yake baadaye walihamia nchini Qatar ambapo anaendelea na elimu yake.

Kukamatwa kwake kuliibua hasira na huruma, huku watumizi wa mtandao wa kijamii wa Twitter wakitumia #StandWithAhmed kutoa tetesi zao.

Mawakili wake wanadai dola milioni 10 kutoka kwa mji wa Irving na dola milioni 5 kutoka kwa shule ya Irving Independent School District, wakisema Ahmed alifedheheshwa peupe na akaathirika kisaikolojia.

Kando na fidia, mawakili wake wanadai kuombwa msamaha, wakisema baada ya tukio hilo, Ahmed amekuwa akipokea jumbe za vitisho na kuwa anahofia usalama wake, swala linalomletea matatizo ya kisaikolojia.

Mawakili hao wanasema watapeleka kesi ya kiraia mahakamani iwapo shule hiyo haitotimiza matakwa ya Ahmed kwa muda wa siku 60.

"maafisa wa polisi wa Irving waligundua kwa haraka kuwa saa hiyo haingedhuru yeyote. Saabu pekee ya kufanya walichofanya ni kwa sababu watu wazima waliohusika bila umakini, walidhani Ahmed alikuwa mvulana hatari kutokana na asili yake, taifa lake na dini". Mawakali wanasema kwenye barua walioandikia mji wa Irving.

Ahmed aliambia wanahabari kuwa kwa wakati huo "ilisikitisha" kuwa mwalimu wake alidhani kuwa saa yake ilikuwa tisho.