Wasifu wa Papa Francis na unyenyekevu wake

Papa Francis Haki miliki ya picha Getty
Image caption Papa Francis hupenda sana kutangamana na watu wa kawaida

Papa Francis ndiye kiongozi wa kwanza wa Kanisa katoliki kutoka mataifa ya Amerika.

Kiongozi huyu alizaliwa mjini Buenos Aires, Argentina 17 Desemba mwaka 1936 na kupewa jina Jorge Mario Bergoglio. Babake, Mario, alikuwa mhasibu katika shirika la reli nchini humo. Mamake Bi Regina Sivori alikuwa tu mke nyumbani aliyeshughulisha zaidi na kuwalewa watoto wake watano.

Ujanani Papa Francis alipenda sana kandanda na aliwahi kufanya kazi za kawaida kama kuwa mlinzi katika jumba la starehe. Na katika shughuli zake za kidini kuna wakati viongozi wa kisiasa wa Argentina walimtaja kama mpinzani wao kisiasa.

Haki miliki ya picha AP

Papa Francis anajiita mtu wa kawaida, msemo wake maarufu na ambao ameutumia mara kadhaa ni kwamba, "watu wangu ni maskini na mimi ni mmoja wao".

Si jambo la kushangaza, hivyo basi, kwamba kiongozi huyo ya Wakatoliki bilioni 1. 4 anaishi maisha ya kawaida sana na katika nyumba ya kawaida makao makuu Vatican. Huwa anajipikia mwenyewe chakula chake.

Papa Francis hata kabla ya kuwatazwa kwake na kuwa kiongozi ya Wakatoliki duniani, katika huduma zake za kidini alionekana kama mtu wa kawaida sana, mpenda maskini na watu wa kawaida na asiyetaka makuu.

Hata mavazi yake ya kidini sio yale yaliyo na mapambo mengi.

Hii ni kutokana na kwamba yeye ni wa huduma ya Wa-Jesuit. Wafuasi wa huduma hii ni makasisi waliojitilea kuishi maisha ya umaskini na kuwahudumia zaidi maskini na wasiojiweza miongoni mwa jamii.

Kabla ya kuingilia shughuli za kidini na hatimaye kujiunga na chuo cha mafunzo ya kidini, kiongozi huyo aliwahi kufanya kazi katika maabara na pia kama mlinzi katika jumba moja la starehe huko Argentina. Na baadaye akiwa na umri wa miaka 33 alitawazwa kuwa kasisi wa Kanisa Katoliki

Haki miliki ya picha AP
Image caption Papa Francis alipokutana na kiongozi wa zamani wa Fidel Castro

Hatimaye alipanda na kuwa Askofu wa jimbo la Buenos Aires mwaka 1998 na miaka miatatu baadaye Papa John Paul II alimtawaza kuwa Kadinali.

Alipokuwa Kadinali serikali za Rais Néstor Kirchner na mrithi wake Cristina Fernández de Kirchner zilimuona kiongozi huo wa kidini kama mpinzani wao kisiasa. Tangu enzi hizo hadi wa leo Papa Francis msimamo wake ni kwamba "Ukimfuata Kristo lazima ufahamu kuwa kuwanyanyasa watu au kuwanyima haki zao ni dhambi kubwa sana.”

Viongozi kadhaa wa dini na madhehebu mengine wamemtaja Papa Francis kama kiongozi mwenye kupenda uhusiano bora miongoni mwa dini na madhehebu tofauti. Kwa mfano mwezi Novemba mwaka 2012 katika Kanisa kuu la Kikatoliki mjini Buenos Aires, Papa Francis aliwaleta pamoja viongozi wa Kiyahudi, Waislamu na madhehebu ya kiinjilisti katika ibada maalum ya pamoja ya kuombea amani na suluhu ya machafuko Mashariki ya Kati.

Haki miliki ya picha
Image caption Papa Francis na mtangulizi wake Papa Benedict XVI

Na ndio pengine tarehe 13 Machi, 2013 alipochaguliwa kuwa kiongozi wa Wakatoliki wote duniani viongozi wa Kiislamu mjini Buenos Aires walisifu uteuzi wake na kumtaja kama " rafiki wa Waislamu na mtu anayependa kushauriana na watu wa dini zote".