Hali CAR bado ni hatari Papa anaposubiriwa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Katika baadhi ya maeneo Bangui, huwezi kuzuru bila kulindwa vikali

Jamhuri ya Afrika ya kati imekumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa miongo kadhaa sasa huku vikosi vya umoja wa matiafa vya kulinda amani vikijaribu kuingilia kati.

Si jambo la kushangaza kwa taifa hili kukumbwa na vurugu ya umwakigaji damu, lakini mkondo wa kidini ambao mapigano hayo yamechukuwa ndilo swala geni katika mzozo huu unaozidi kuenea.

Usalama katika mji mkuu wa Bangui ni mbaya, na ni hatari kwa Papa Francis kuja hapa.

Na bila shaka ukosefu wa usalama mjini Bangui ndiyo changamaoto kubwa kwa vyombo vya dola chini ya rais wa mpito Catherine Samba Panza, na walinda uslama wa Vatican.

Tayari polisi wa Vatican wamepiga kampi mjini Bangui ambako wanaendesha upekuzi wa kiuslama katika maeneo ambayo Papa Francis anatarajiwa kuzuru. Lengo hasa la ziara ya kiongozi huyo wa kanisa katoliki ulimwenguni ni kuleta uwiano wa kidini miongoni mwa makundi hasimu ya wakristo na waislamu.

Wapanga ratiba tayari wamefanikiwa kuwahusisha viongozi kadhaa wa kidini katika maandalizi yao ikiwa pamoja na askofu, imamu na mwakilishi wa papa nchini humo, askofu mkuu Fanco Coppola.

Baadhi ya Waislamu ambao wameathirika na mapigano hayo wamepewa hifadhi katika kanisa moja lenye ukuta mrefu mjini Bangui.

Lakini mji uliogawanyika zaidi kwa misingi ya kidini ni Bambari.

Mto umegawanya mji huu katika sehemu mbili zinazomilikiwa na wapiganaji wa makundi ya Seleka na Anti-Balaka.

Ingawa mzozo huu umechukuwa mkoondo wa kidini, wengi wanaamini kwamba chimbuko la uhasama katika jamhuri ya afrika ya kati ni kung'ang'ania uongozi wa kisiasa na uthibiti wa rasilimali kama vile dhahabu na almasi ambayo imetabakaa kote nchini humo.

Maandalizi ya kumkaribisha papa Francis yanaendelea vizuri. Watu wengi, kando ya misimamo yao ya kidini, wanamtaka papa Francis azuru na wako tayari kumkaribisha katika Jamhuri ya Afrika ya kati.