Meli ya Iran yatekwa nyara Somalia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maharamia wa Somalia

Maharamia wa Somalia wameiteka nyara meli moja ya Iran ikiwa na wafanyi kazi 15.

Hayo yamesemwa na maafisa wakuu nchini Somalia pamoja na wataalam wa maswala ya baharini.

Meli hiyo ya Iran iliyokuwa na wavuvi 15 ilitekwa nyara siku ya Jumatatu, licha ya tahadhari iliyokuwa imetolewa awali kuwa kuna uwezekano wa maharamia kuanza tena shughuli zao potovu katika maeneo ya bahari Hindi.

Hata ingawa kumeshuhudiwa visa vidogo vidogo vya uharamia katika maeneo ya bahari hiyo karibu na ufuo wa Somalia, visa vya utekaji nyara vimepungua mno katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Maharamia wa Somalia

Hiyo ni kutokana na kampuni za usafiri wa baharini kukodisha walinda usalama wa kibinafsi pamoja na kuongezeka kwa manowari za kijeshi za mataifa mbalimbali ya dunia zikipiga doria katika maeneo hayo ya Somalia na upembe wa Afrika.

Meli hiyo ilidhibitiwa na maharamia hao usiku wa kuamkia Jumatatu katika maeneo ya baharini karibu na mji wa Somalia wa Eyl.

Hayo ni kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa idara ya kukabiliana na maharamia na waziri wa bandarini wa jimbo la Somalia lililojitenga la Puntland, bwana Abdirizak Mohamed Dirir.

Haki miliki ya picha
Image caption Haramia wa Somalia

Bwana John Steed, ambaye ni maneja mkuu wa kundi moja la Afrika mashariki la Oceans Beyond Piracy, amethibitisha kutekwa kwa meli hiyo ya Iran iitwayo, Muhammidi.

Meli nyengine mbili za wavuvi wa Iran, zilitekwa nyara mwezi Machi mwaka huu.