Papa Francis awasili Kenya

Bofya hapa kwa habari za karibuni zaidi

19:02 Papa Francis amemaliza hotuba yake, akasalimia baadhi ya wageni wa heshima na kisha kuondoka ukumbini.

19:00 Papa Francis: "Nawashukuru tena kwa kunikaribisha vyema, na kwenu na familia zenu, na watu wote wa Kenya, ziwe baraka tele za Mwenyezi Mungu.”

Mungu abariki Kenya!"

18:59 Papa Francis: “Nawahimiza kuwajali maskini, ndoto za vijana, na kugawana vyema maliasili na nguvu kazi ambazo Mola amelipa taifa lenu. Nawahakikishia kuendelea kwa juhudi za kanisa Katoliki, kupitia kazi zake za elimu na kusaidia jamii, kutoa mchango katika hili.”

18:58 Papa Francis: “Historia inaonyesha kuwa ghasia, mizozo na ugaidi huchochewa na kuogopana, kutoaminiana na kutamauka ambako husababishwa na umaskini na kupoteza matumaini. Vita dhidi ya maadui wa amani na ustawi vinafaa kuendeshwa na wanaume na wanawake wanaoamini katika, na kushahidia, maadili makuu ya kidini na kisiasa ambayo yalipelekea kuasisiwa kwa taifa.”

18:57 Papa Francis: “Jamii zetu zinapoendelea kukumbwa na migawanyiko, ya kikabila, kidini au kiuchumi, binadamu wote wenye nia njema wameitwa kufanyia kazi maridhiano, msamaha na uponyaji. Katika juhudi za kuunda mfumo wa demokrasia, kuimarisha utangamano na uwiano, kuvumiliana na kuheshimiana, lengo kutenda mema linafaa kuwa ndilo kuu.”

18:54 Papa Francis: “Kenya imebarikiwa sio tu na umaridadi, katika milima, mito na maziwa, misitu, nyika na maeneo kame, bali pia katika utajiri wa maliasili. Wakenya wamethamini sana zawadi hizi kutoka kwa Mungu na wanajulikana kwa utamaduni wao wa kuhifadhi (mazingira). Mgogoro wa kimazingira unaokumba dunia kwa sasa unahitaji kutambua zaidi uhusiano kati ya binadamu na maumbile.”

18:51 Papa Francis: “Taifa lenu pia lina vijana wengi. Siki hizi nitakazokuwa hapa, nasubiri sana kukutana na wengi wao, kuzungumza nao na kuwapa matumaini katika ndoto zao za siku za usoni.”

18:53 Papa Francis:“Kenya ni taifa changa na linalokua na lenye jamii mseto na limekuwa likitekeleza jukumu muhimu kanda hii. Kwa njia nyingi, mnayopitia katika kuunda demokrasia yamekuwa yakipitiwa na mataifa mengi Afrika.”

18:51 Papa Francis: “Nashukuru sana kwa kunikaribisha vyema, kwenye ziara yangu ya kwanza Afrika.”

18:50 Papa Francis anasalimiana na Rais Kenyatta. Anaanza kuhutubu.

18:50 Rais Kenyatta: Nakukaribisha uhutubie Wakenya".

18:39 Papa Francis na Rais Kenyatta waingia ukumbini ikulu ya Nairobi. Rais Kenyatta anamkaribisha Papa Francis Kenya. Rais Kenya amegusia kwamba kesho ni siku ya maombi ya taifa Kenya.

18:17 Kabla ya kuingia mkutanoni, Papa Francis, anayejulikana sana kwa kuthamini mazingira, amepanda mti ikulu, kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation.

18:16 Papa Francis kwa sasa anakutana na Rais Kenyatta ikulu ya Nairobi. Baadaye anatarajiwa kutoa hotuba.

17:44 Papa Francis anapigiwa mizinga 21 ambayo kawaida hutumiwa kulaki kiongozi wa taifa jingine. Papa Francis ndiye kiongozi wa Vatican.

17:40 Papa Francis awasili Ikulu, Nairobi na kulakiwa na Rais Uhuru Kenyatta.

17:28 Rais Kenyatta amewasili ikulu ya Nairobi. Papa Francis yuko njiani kuelekea huko ambapo atakaribishwa rasmi Kenya.

17:25 Hivi ndivyo Papa Francis alivyoandika kwenye kitabu uwanja wa ndege wa JKIA: "na maombi na shukrani kwa kuwatunza wasafiri."

Haya ni kwa mujibu wa Nexus Kenya, idara ya habari ya serikali ya Kenya.

Haki miliki ya picha Nexus Kenya

17:15 Papa Francis aingia kwenye gari lake na kuondoka.

17:09 Wageni wanajiandaa kuondoka uwanja wa ndege wa JKIA. Papa Francis anatarajiwa kuelekea Ikulu kukaribishwa rasmi nchini na Rais Kenyatta.

16:53 Kwaya inaimba "Karibu Kenya Papa Francis"

Haki miliki ya picha Reuters

16:52 Alakiwa kwa shangwe na nderemo. Amsalimia Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Haki miliki ya picha Reuters

16:52 Papa Francis ashuka kutoka kwenye ndege.

Haki miliki ya picha Other

16:50 Wanahabari walioandamana na Papa Francis watangulia kushuka kutoka kwenye ndege.

16:41 Viongozi wa Kanisa Katoliki wakiwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta wamejiandaa kumlaki Papa Francis atakaposhuka kutoka kwenye ndege iliyombebea, ambayo ni kutoka shirika la ndege la Italia, Alitalia.

16:33 Ndege iliyombeba Papa Francis yatua uwanja wa ndege wa JKIA, Nairobi.

16:25 Ndege iliyombeba Papa Francis kwa sasa imo kwenye anga ya Kenya.

16:25 Rais Kenyatta ameelekea uwanja wa ndege wa JKIA kumlaki Papa Francis ambaye anatarajiwa kuwasili wakati wowote baada ya saa kumi unusu alasiri.

16:20 Mabango yamewekwa katika barabara mbalimbali kumkaribisha Papa Francis Kenya

16:08 Papa Francis aandika kwenye Twitter: "Mungu abariki Kenya".

15:07 Papa Francis amezungumza na wanahabari walioandamana naye kwenye safari ya ndege kutoka Roma kuelekea Nairobi.

Haki miliki ya picha Reuters

“Ninaenda Kenya, Uganda na kwa ndugu zangu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati nikiwa na furaha,” shirika la habari la Reuters limemnukuu akisema.

Haki miliki ya picha AP

“Tutumai kuwa ziara hii itazalisha matunda mema, kiroho na kimwili.”

Haki miliki ya picha Reuters

12:36 Huyu hapa ni Papa Francis akiabiri ndege. Ndege yake ishaondoka uwanja wa ndege wa Fiumicino, Roma kuelekea Nairobi Kenya.

Haki miliki ya picha AFP

12:11 Wakenya wanaendelea kujiandaa kumpokea Papa Francis baadaye leo. Barabarani na katika majumba, kuna mabando ya kumkaribisha Papa.

10:47 Magazeti ya Kenya yalivyoandika kuhusu ziara ya Papa Francis.

10:39 Makundi mbalimbali yamekuwa yakijiandaa kumlaki Papa Francis. Mfano ni watoto hawa kutoka kanisa la St Martin.

Huwezi kusikiliza tena

Hii hapa nayo ni kwaya ya pamoja ambayo itamwimbia Papa Francis.

Huwezi kusikiliza tena

10:33 Ndege ya Papa Francis imepaa kutoka uwanja wa ndege wa Fiumicino, Roma, ikiwa imechelewa kwa karibu robo saa. Anatarajiwa kuwasili uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta saa 17:00.

10:00 Hujambo! Karibu tukupashe yanayojiri katika ziara ya Papa Francis barani Afrika ambayo itamfikisha Kenya, Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati.