Watanzania kwenda kumuona Papa Francis

Image caption Baadhi ya Watanzania wanasafiri kwenda Uganda kumuona Papa Francis

Kiongozi mkuu wa Kanisa katoliki duniani, Papa Francis wa kwanza anaanza ziara yake leo barani Afrika akitembelea Kenya, Uganda na Afrika ya kati.

Pamoja na kwamba Baba mtakatifu huyu, hatatembelea Tanzania katika ziara yake ya bara la Afrika , lakini baadhi ya Wakrista wa taifa hilo wana shamra shamra na wengine hasa wale wa Imani ya Kikatoliki wameamua kwenda japo mahali pamoja tu atakapokuwa kiongozi wa Wakatoliki wapatao 1.4 bilioni.

Baadhi ya Watanzania hao wameamua kusafiri hadi Namugongo, nchini Uganda.

Lakini waumini hao wameamua kwenda hadi katika kituo hicho cha Namugongo, huko Uganda wakati Papa Francis anazuru bara la Afrika wakiwa wana sababu tofauti tofauti.

Paula Protas anasema: "Mimi ameamua kwenda Uganda kwa sababu hii ni mara yangu ya tatu kwenda kuhiji na naona hii ni nafasi ya kipekee kwangu kwa sababu Baba Mtakatifu anakuja kufanya hijja kule kwa ajili ya wale mashahidi. Kwa hivyo nliona ni vyema na mimi niende kwa kuwa kule kuna mambo mengi mazuri kwa sisi Wakatoliki".

Flowin Madiwa yeye hii ni mara ya tisa mfululizo kwenda nchini Uganda kwa ajili ya hija.

Kwa sababu kuna kumbukumbu ya mashahidi wa Uganda kila mwaka, ibada inayofanyika Namugongo huwa inamvutia sana na kumgusa sana.

"Nimejiwekea nadhiri kwamba Mungu akinipa uzima nitakuwa nikienda kila mwaka. Hata ujio wa Baba Mtakatifu unanipa msukumo zaidi,” alimwambia mwandishi wa BBC Esther Namuhisa.

Ingawa kituo cha Namugongo ni miongoni mwa hamasa katika safari ya waumini hao kuelekea Uganda, hamu na hisia mbalimbali zimetawala kwa waumini wa Kikatoliki nchini Tanzania.

Image caption Baadhi ya makanisa yana jina la mashahidi wa dini kutoka Uganda

Ujio wa Baba Mtakatifu umegonga vichwa vya habari kwa wengi kwa kuleta matumaini kuwa Afrika imekumbukwa.

Idadi ya wanawake wanaopanga kusafiri ni kubwa, wengine wao wakisema ni lazima wafike huko licha ya umri.

Image caption Umri si hoja kwa Bi Edward anayesema majuzi alisafiri hadi Israel

Bi Magaret Edward kutoka kaskazini mwa Tanzania, ana umri wa miaka 70, na anasema umri wake haujalishi kwa kuwa aliwahi kwenda Israel miaka miwili iliyopita kuhiji na kwa hivyo hawezi kukosa kwenda kumuona Papa huko Uganda.

Ujio huu wa Papa pia umerahisisha nia za wengi ambao walikuwa wanatamani kwenda Roma kumuona, hivyo kuja kwake katika mataifa ya jirani ni nafuu kwao.

Wamekua wakifuatilia ujio huo kwa karibu na wengine hata hivyo waumini hawa kutoka Tanzania wamejawa na matumaini na hisia mbalimbali

Image caption Parokia Watakatifu Mashahidi wa Uganda eneo la Magomeni, Tanzania

“Nanyi mtakuwa mashahidi wangu," ndiyo kauli mbiu ya hija ya Baba Mtakatifu nchini Uganda.

Ataangazia zaidi kuendeleza mchakato wa kulinda, kutetea na kudumisha haki, amani na upatanisho kati ya wananchi .