Ukraine yafunga anga yake kwa Urusi

Haki miliki ya picha RIA Novosti
Image caption Ukraine imefunga anga yake kwa ndege zote za Urusi.

Ukraine imefunga anga yake kwa ndege zote za Urusi.

Aidha nchi hiyo imefuta kandarasi zote za ununuzi wa gesi ilizoandikisha na Urusi.

Kauli hii inafwatia kuzimwa kwa umeme kutoka Ukraine kwenda jimbo lililomeguliwa la Crimea.

Crimea imekuwa bila umeme kuanzia mwishoni mwa juma baada ya nyaya zinazosambaza umeme kulipuliwa na watu wasiojulikana.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kampuni ya nishati ya Urusi Gazpron imeacha kupeleka gesi nchini Ukraine wakisema sababu ni kuwa nchi hiyo haijailipia gesi hiyo.

Urusi inailaumu Ukraine kwa matukio hayo huku Ukraine ikilaumu waasi wa Tartar.

Wakati huohuo kampuni ya nishati ya Urusi Gazpron imeacha kupeleka gesi nchini Ukraine wakisema sababu ni kuwa nchi hiyo haijailipia gesi hiyo.

Usafirishaji wa gesi ulirejelewa mwezi uliopita katika makubaliano ambayo yaliitaka Ukraine kuilipa gesi hiyo mapema.

Usafirishaji wa gesi umesitishwa mara kwa mara tangu mzozo kuibuka kati ya Urusi na Ukraine uliosabaishwa na hatua ya Urusi ya kulimega eneo la Crimea lililokuwa Ukraine.

Haki miliki ya picha UKRINFORM
Image caption Crimea imekuwa bila umeme kuanzia mwishoni mwa juma baada ya nyaya zinazosambaza umeme kulipuliwa na watu wasiojulikana.

Mkuu wa Gazprom anaonya kuwa usafirisha wa gesi kwenda nchi za ulaya kupitia nchini Ukraine utaathiriwa.

Kwa sasa Ukraine imesitisha shughuli zozote za kibiashara na Crimea.

Kwa upande wake Urusi imetishia kusimamisha ununuzi wa bidhaa za Ukraine.