Watoto wanaozaliwa wikendi hufariki zaidi UK

Image caption Watoto wanaozaliwa wikendi nchini Uingereza hufariki sana ikilinganishwa na wale wanaozaliwa siku za juma

Watoto waliozaliwa wikendi iliopita nchini Uingereza wana hatari kubwa ya kufariki ikilinganishwa na wale waliozaliwa siku za juma,kulingana na watafiti.

Utafiti uliofanyiwa zaidi ya watoto milioni 1.3 waliozaliwa umebaini kwamba kuna vifo 7.1 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa wikendi.

Hii ni asilimia 7 zaidi ikilinganishwa na siku za juma.

Taasisi ya Imperial mjni London imesema kuwa iwapo siku zote zingekuwa na viwango sawa vya vifo kama vile siku ya Jumanne,ambayo ina viwango vya chini kungekuwa na vifo 770 vichache kwa mwaka.

Watafiti hao wamesema kuwa huku viwango vya vifo vikiwa chini,tofauti hiyo ni muhimu na kuzua wasiwasi kuhusu viwango vya utunzaji wikendi.

Image caption mtoto aliyezaliwa

Mnamo mwezi Septemba ,utafiti tofauti ulibaini kwamba wagonjwa waliolazwa ili kuhudumiwa wakati wa wikendi walikuwa na hatari zaidi ya kufariki katika kipindi cha siku 30 ikilinganishwa na wale waliolazwa katika siku za juma.

Utafiti huo umetumiwa na mawaziri katika harakati zao za kutaka kuongeza huduma wakati wa wikendi,sera ambayo imezua mgogoro baina yao na madaktari na kusababisha madaktari wapya kupiga kura wakiunga mkono kufanya mgomo kuanzia juma lijalo.

Utafiti huo mpya,uliochapishwa na jarida la matibabu la Uingereza uliangazia visa vya watoto wanaofariki wakiwa tumboni kati ya kipindi cha siku saba wakiwa hospitalini kutoka mwaka 2010 hadi 2012.