Mshauri wa Nkurunziza anusurika shambulio

Haki miliki ya picha Burundi Police
Image caption Watu zaidi ya 200 wameuawa nchini Burundi tangu Aprili

Mshauri wa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amenusurika shambulio alipokuwa akitoka nyumbani kwake katika eneo la Kajaga, magharibi mwa mji mkuu Bujumbura, polisi wanasema.

Zenon Ndaruvukanye alinusurika bila majeraha yoyote, lakini mlinzi wake, ambaye alikuwa afisa wa polisi, alifariki kutokana na majeraha ya risasi.

Washambulijai walitoroka wakitumia gari aina ya Toyota lakini polisi walipashana habari na gari lao likazuiwa maili kadha kutoka Kajaga. Waliacha gari hilo na kutorokea soko lililo karibu, lakini mwishowe wawili walikamatwa. Mmoja wao alifanikiwa kutoroka.

Gari hilo aina ya Toyota lilipatikana na silaha mbalimbali zikiwemo bunduki aina ya AK47 na guruneti.

Haki miliki ya picha Burundi Police

Polisi baadaye walipelekwa kwenye nyumba moja viungani mwa mji wa Bujumbura ambapo walipata silaha zaidi.

Mji wa Bujumbura umekumbwa na machafuko ambayo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 200 tangu Aprili.