Papa Francis ahimiza vijana wakabili rushwa

Image caption Papa Francis amekuwa akisisitiza umuhimu wa vijana kwa taifa

Papa Francis amehutubia maelfu ya vijana nchini Kenya na kuwahimiza wasijihusishe na ufisadi na ukabila.

Akihutubu katika uwanja wa michezo wa Kasarani, Nairobi Papa Francis amesema vijana wanaweza kuchangia katika kukabiliana na changamoto hizo, ambazo zimelaumiwa kwa kukwamisha maendeleo katika mataifa ya Afrika.

“(Ufisadi) Ni kama sukari, tamu, twaipenda, ni rahisi. Kisha, tunaishia kuumia. Sukari inaweza kuzidi hivi kwamba tunapata kisukari, au taifa letu linaishia kuwa na kisukari,” amesema.

"Nawasihi, msiipende sukari hiyo iitwayo ufisadi. Katika ufisadi, sawa na katika kila jambo, lazima uchukue msimamo. Ufisadi si njia ya uhai, ni njia ya mauti.”

Kadhalika, aliwahimiza wasijihusishe na ukabila na kuwataka wawatazame watu wengine kama raia wa taifa moja.

Papa Francis pia amewashauri Serikali zihakikishe vijana wanapata elimu na ajira, akisema ndiyo njia pekee ya kuwazuia kujiingiza katika makundi yenye itikadi kali.

Kwa mara nyingine, ameelezea umuhimu wa familia kama nguzo kuu katika jamii.

Maelfu ya vijana walikuwa wamejitokeza kwa hotuba ya Papa Francis na baadhi hawakupata nafasi ya kuingia ndani ya uwanja.

Huwezi kusikiliza tena

Awali, apotembelea mtaa duni wa Kangemi, alikemea unyakuzi wa ardhi na dhuluma wanazotendewa watu maskini mijini akisema wana haki sawa ya kupata huduma bora.

“Ninafahamu kuhusu tatizo kubwa linalosababishwa na wastawishaji wasio na sura ambao hujitwalia ardhi na hata kujaribu kunyakua viwanja vya kuchezea vya watoto wenu shuleni. Hili ndilo hufanyika tunaposahau kwamba Mungu aliwapa watu wote ardhi, waitumie kwa maisha yao, bila kutenga au kupendelea yeyote," aliwaambia.

Papa Francis anatarajiwa kuondoka Nairobi baadaye leo kuelekea Uganda.