Papa amewasili Jamhuri ya Afrika ya Kati

Image caption Papa Francis ameanza mkondo wake wa mwisho wa ziara yake katika mataifa ya Afrika

Papa Francis ameanza mkondo wake wa mwisho wa ziara yake katika mataifa ya Afrika Jumapili kwa kuwasili katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Bangui

Kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani aliwasili mjini Bangui muda mchache uliopita na kulakiwa kwa shangwe na nderemo na maelfu ya wakatoliki.

Aidha Papa Francis ametangaza nia yake kuu ni kuleta amani katika taifa hilo ambalo limekumbwa na mapigano ya kidini kati ya Waiislamu na Wakristo

Licha ya hofu ya usalama wake katika taifa hilo, Papa amesema ana moyo wa kutuma ujumbe wa amani na matumiani.

Image caption Maelfu ya wakristo walisimama mabarabarani kumlaki papa Francis

Papa Francis anafanya ziara yake ya kwanza katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ikiwa sehemu ya mwisho ya safari yake Afrika.

Papa aliwaambia wakaazi wa kambi ya wakimbizi katika mji mkuu, Bangui, kwamba anawatakia amani.

"lakini amani haiwezekani bila ya upendo, bila ya kuvumiliana, bila ya kusamehena. Kila mtu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, anaweza kusaidia kuleta amani kati yetu, alisema Papa

Image caption Papa francis alilakiwa na rais Catherine Samba katika uwanja wa ndege mjini Bangui

''Ingawa kuna tofauti ya dini, utamaduni na tabaka.Sote tunaweza kuishi kwa amani ikiwa sote ni ndugu. Nitapenda sote tuwe ndugu, ili kuweza kuleta amani." alisema Papa

Ziara ya papa Francis imewadia muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuleta amani mwezi ujao.

Mbali na kuadhimisha misa katika mji mkuu wa Bangui, Papa anatarajiwa kukutana na viongozi wa Kiislamu na kutembelea msikiti mmoja mjini humo katika kitongoji kilichoathirika sana na mapigano cha PK5.

Papa Francis amekuwa katika ziara yake ya kwanza tangu atawazwe kuwa kiongozi wa wakatoliki duniani iliyoanzia Kenya Uganda na sasa inakamilikia Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Image caption Usalama umeimarishwa mjini Bangui

Jamhuri ya Afrika ya kati:

  • Idadi ya watu : 4.6 million - 50% Wakristo, 15% Waislamu, 35% imani zingine
  • Imemkubwa na vita miaka na uongozi mbaya
  • Mapigano yameegemea imani na dini majuzi
  • Ilitawaliwa awali na mfalme Jean-Bedel Bokassa
  • Inautajiri mkubwa wa almasi
  • Inawalinda usalama wa umoja wa mataifa 10,000- tangu Septemba 2014
  • Ufaranza ndio iliyoitawala wakati wa Ukoloni
  • Ufaransa inawanajeshi 2000 huko tangu Decemba 2013