Rais wa zamani wa Guinea akiri mashtaka US

Konate Haki miliki ya picha AFP
Image caption Konate alikuwa rais wa mpito wa Guinea 2010

Jenerali wa zamani wa kikosi cha Muungano wa Afrika ambaye aliwahi kuhudumu kama rais wa mpito nchini Guinea amekiri mashtaka ya kulangua maelfu ya dola Marekani.

Viongozi wa mashtaka wanasema Sekouba Konate, 51, alijaribu kuingia na $64,000 (£42,400), nchini Marekani alipokuwa safarini kutoka Ethiopia hadi uwanja wa ndege wa Dulles mwaka 2013. Sehemu kubwa ya pesa hizo alizificha mkobani.

Jenerali Konate alihudumu kama kaimu kiongozi wa Guinea wakati wa mzozo wa kisiasa uliokumba taifa hilo la Afrika Magharibi 2010.

Baadaye aliteuliwa na Muungano wa Afrika kama “mwakilishi mkuu” katika juhudi za kuunda kikosi cha akiba cha muungano huo cha kutumiwa kutatua mizozo Afrika.

Alikuwa amepangiwa kufika kizimbani Marekani Jumanne kujitetea. Hata hivyo, alikiri mashtaka na sasa huenda akafungwa hadi miaka mitano jela, shirika la habari la Associated Press limeripoti.

Kwa mujibu wa taarifa aliyotia saini kama sehemu ya kukiri makosa, jenerali huyo amesema ilikuwa makosa kupekua mizigo yake ikizingatiwa hadhi yake kama kiongoni wa zamani wa Guinea na kamanda wa vikosi vya AU, nyaraka za mahakama zinaonyesha, shirika la Reuters limeripoti.