Mwingereza Jermaine Grant afungwa jela Kenya

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Jermaine alikamatwa mjini Mombasa 2011

Mwanamume mmoja raia wa Uingereza, anayetuhumiwa kupanga mashambulio ya kigaidi, amefungwa jela miaka tisa na mahakama mjini Mombasa.

Jermaine Grant, anayetoka London, amefungwa jela kwa makosa tisa yanayohusiana na kujaribu kujipatia uraia wa Kenya kwa njia haramu.

Bado anakabiliwa na mashtaka ya "kupanga kuunda vilipuziā€ kwenye kesi ambayo bado inaendelea mjini Mombasa. Grant amekanusha mashtaka hayo.

Mwingereza huyo alikamatwa 2011, pale betri na kemikali vilipopatikana nyumbani kwake Mombasa.

Polisi nchini Uingereza, ambao wamewasaidia maafisa wa Kenya katika uchunguzi, wanadai vifaa hivyo vilikuwa vya kutumiwa kuunda vilipuzi.

Samantha Lewthwaite, ajulikanaye sana kama "White Widow," (Mjane Mweupe), ambaye anasakwa kuhusiana na mashambulio ya 7/7 nchini Uingereza pia anadaiwa kuhusika katika njama hiyo.

Hukumu dhidi ya Grant imetolewa baada yake awali kuondolewa mashtaka hayo tisa yaliyohusiana na kujaribu kujipatia uraia wa Kenya kinyume cha sheria mapema mwaka huu.

Hata hivyo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Mombasa, alibatilisha uamuzi huo na akamhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kila kosa.