Wanne wauawa Pakistan kuhusiana na mauaji Peshawar

Peshawar Haki miliki ya picha AP
Image caption Mji wa Peshawar uko karibu na Afghanistan

Pakistan imewanyonga watu wanne waliohusishwa na shambulio katika shule ya jeshi eneo la Peshawar lililoua watu zaidi ya 150, wengi wao watoto.

Wanaume hao walihukumiwa kifo na mahakama ya kijeshi na ndio wa kwanza kunyongwa kuhusiana na shambulio hilo.

Wanamgambo wa Taliban walishambulia shule ya Army Public School kaskazini magharibi mwa jiji la Peshawar Desemba 16, 2014.

Kuuawa kwa wanne hao kumetokea wiki nne tu kabla ya maadhimisho ya miaka mine tangu kutokea kwa shambulio hilo lililotikisa taifa hilo.

Serikali ilijibu kwa kukabiliana vikali na wapiganaji hao wa Kiislamu, na kuunda mahakama za kijeshi kuwafungulia mashtaka washukiwa wa ugaidi na pia kuanza kutekelezwa kwa hukumu ya kifo baada ya kusitishwa kwa miaka sita.

Mapema wiki hii, mkuu wa jeshi Jenerali Raheel Sharif alitia saini vibali vya kuuawa kwa wanne hao Maulvi Abdus Salam, Hazrat Ali, Mujeebur Rehman and Sabeel.

Maafisa wamesema waliuawa mapema Jumatano asubuhi katika gereza lililo mji wa kaskazini magharibi wa Kohat.