UN yalaumu serikali na upinzani Burundi

Burundi Haki miliki ya picha Burundi Police
Image caption Serikali imekuwa ikiendesha operesheni ya kuwapokonya raia silaha

Umoja wa Mataifa umesema wakuu wa serikali ya Burundi na viongozi wa upinzani wanajaribu kuigawanya nchi hiyo kwa misingi ya kimbari.

Mshauri maalum wa umoja huo kuhusu mauaji ya kimbari Adama Dieng amesema matamshi yanayotolewa ni sawa na yaliyokuwa yakitolewa kabla ya kutokea kwa mauaji ya kimbari katika taifa jirani la Rwanda 1994.

Bw Dieng ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati.

Watu 240 wameuawa nchini humo tangu Rais Pierre Nkurunziza atangaze atawania urais kwa muhula wa tatu mwezi Aprili. Alishinda uchaguzi.

Msemaji wa serikali Willy Nyamitwe, ametetea serikali akisema inakabiliana na magaidi.

“Mashambulio ya kigaidi yanaweza kutokea Burundi na pahali popote duniani. Hii haina maana kwamba Burundi haina amani,” Bw Nyamitwe amesema.

Image caption Mwanamke huyu alikuwa amebeba bango wakati wa ibada Nairobi kumuomba Papa Francis aisaidie Burundi

“Tunapigana dhidi ya watu wanaojaribu kuleta ukosefu wa usalama nchini mwetu. Tunawapokonya raia silaha ambazo wanashikilia kinyume cha sheria, lakini baadhi wanafanya mambo kama magaidi. Kwa hivyo hili halifanyiki Burundi pekee, hata Ulaya, na Marekani.”

Msemaji huyo amesema wapinzani wanaua wafuasi wao ili kuiharibia sifa serikali.

“Wanajua wapinzani wakiuawa, watu watadhani ni serikali inayowaua,” amesema Bw Nyamitwe.