Uchina yaahidi $6.5bn kwa Afrika Kusini

Xi Haki miliki ya picha XINHUA
Image caption Bw Xi alikutana na Rais Zuma Jumatano

Uchina na Afrika Kusini zimetia saini mikataba na mikopo ya thamani ya $6.5bn (£4.3bn), inayoangazia zaidi miundo mbinu.

Mikataba hiyo ilitangazwa wakati wa ziara ya siku nne ya Rais wa Uchina Xi Jinping inayolenga kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.

Jumla ya mikataba 26 ilitiwa saini Jumatano, $2.5bn zikienda kwa shirika la reli la serikali.

Uchina imetoa msururu wa mikopo kwa nchi za Afrika, ambazo nazo huuzia taifa hilo mafuta na bidhaa nyingine muhimu.

Hata hivyo, idadi ya bidhaa ambazo mataifa hayo huuzia Uchina imekuwa ikipungua.

Uwekezaji wa Uchina Afrika ulishuka asilimia 40 nusu ya kwanza ya mwaka huu, kwa mujibu wa wizara ya uchumi ya Uchina.

Ziara ya Xi imetazamwa na wengi kama hatua ya kuyahakikishia mataifa ya Afrika kwamba Uchina itaendelea kuwekeza katika bara hilo licha ya kupungua kasi kwa ukuaji wa uchumi wa Uchina.

Kabla ya kutua Afrika Kusini, Bw Xi alizuru Zimbabwe Jumanne, ambako pia aliahidi taifa hilo mikopo ya kusaidia kuinua uchumi wake uliodorora.

Haki miliki ya picha Reuters

Bw Xi anatarajiwa kuongoza mkutano mkuu wa ushirikiano kati ya Afrika na Uchina Ijumaa, ambao umepangiwa kuhudhuriwa na viongozi wa mataifa kadha barani.

Ripoti zinasema Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari atamuomba Bw Xi mikopo ya kufadhili miradi ya kawi na reli.