Wadukuzi waandama wanaotumia LinkedIn

Violet Haki miliki ya picha Symantec
Image caption Watu wengi hutarajia kutumiwa barua na waajiri watarajiwa

Wadukuzi wa mitandaoni wameanza kuandama zaidi watu wanaotumia mtandao wa LinkedIn, shirika la usalama wa mtandaoni Symantec linasema.

Uchunguzi wa shirika hilo umebaini kuna akaunti nyingi sana bandia, ambazo zina majina ya watu wanaojidai kuwa wataalamu katika sekta mbalimbali.

Wengi wanajifanya watu wanaotaka kuajiri wafanyakazi, na hivyo basi kuwawezesha wadukuzi kuingia kwenye mitandao ya wataalamu ambao huishia kuwaamini.

Kupitia urafiki huu, wahalifu wanaojidai kuwa waajiri wanaweza kuwashawishi watu kutoa maelezo na taarifa zao za kibinafsi, au kuwaelekeza kwenye tovuti hatari.

Aidha wanawatumia barua pepe zenye nia ya kuiba maelezo ya akaunti zao.

Wengi hunaswa na mtego huu na kufungua barua pepe hizo kwa sababu mtu anapotafuta kazi hutarajia kuandikiwa ujumbe na mwajiri mtarajiwa.

Shirika hilo la usalama linafanya juhudi za pamoja na LinkedIn kufuta akaunti hizo bandia.

Mtafiti kutoka Symantec Dick O'Brien anawashauri wale ambao wanagundua akaunti ambazo wanazishuku uhalali wake wapige ripoti kwa shirika hilo mtandaoni.

Hii si mara ya kwanza kwa wataalamu kueleza hatari zilizopo kwenye mtandao wa kijamii wa LinkedIn.

Oktoba, wataalamu kutoka Dell waligundua akaunti 25 bandia ambazo zilikuwa zimejihusisha na akaunti hadi 200 halali, za watu waliokuwa wakifanya kazi katika sekta za ulinzi, mawasiliano, serikali na utoaji huduma.

Nyingi za akaunti hizo baadaye zilibainika kuwa na uhusiano na kundi la wadukuzi kutoka Iran.