Albino kuwania taji la urembo Tanzania

Albino
Image caption Mshindi wa kitaifa atachaguliwa kutoka kwa washindi wa kanda nne

Watu wenye ulemavu wa ngozi Tanzania wamepata fursa ya kushindania taji la kipekee la urembo, na pia kuhimiza jamii kuthamini utu wao.

Shindano hilo kwa jina Miss Albino Tanzania, ambapo malkia wa urembo wa mwaka huu atatawazwa, limeanza kwa kuteuliwa kwa mshindi wa kanda ya Dar es Salaam.

Katika kanda hiyo, kulikuwa na warembo wanane walioonyesha ulimbwende wao lakini kama kawaida katika kila shindano, mshindi alikuwa mmoja – Bi Priscilla Mluge Samweli, 22.

Kama mshindi, Bi Samweli alitunukiwa Sh 300,000, huku mshindi wa pili, Lilian Msime akiondoka na kitita cha Sh200,000.

Bi Ratifa Abdul, aliyeshika nafasi ya tatu, alirudi nyumbani na Sh100,000.

Image caption Mwandishi wa BBC Tulanana Bohela alikutana na warembo wanane wa Dar es Salaam wakijiandaa kwa shindano

Shindano hilo la kipekee lilifanyika katika ukumbi wa Msasani Club, katika jiji la Dar es Salaam na wananchi waliohudhuria walishangilia washiriki wote.

Shindano hilo la kipekee limeandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Save the Vulnerable Foundation (SVF).

Mwenyekiti wa shirika hilo Bw Fredy Kaula, kama alivyonukuliwa na gazeti la Mwananchi, anasema lengo la shindano hilo ni kuibua na kutambua vipaji, kujenga ujasiri, na kuwawezesha wasichana wenye ulemavu wa ngozi kutimiza malengo yao.

Image caption Ulimbwende wetu 2015/2016 ndio ujumbe ulioandikwa kwenye tisheti zao

Waandalizi wa shindano hilo watatafuta pia mshindi wa kanda za Arusha upande wa kaskazini, Mbeya eneo la kusini na Dodoma katikati mwa Tanzania.

Washindi wa kanda watakutana na shindano kuu Februari mwaka 2016 kumtawaza Miss Albino Tanzania.