Mshangao nyumbani kwa walioua watu California

Haki miliki ya picha ABC NEWS AP
Image caption Tashfeen Malik na Syed Rizwan Farook

Mawakili wanaoiwakilisha familia ya wanandoa wawili walioua watu 14 mjini San Bernardino, California wamesema jamaa za wawili hao wamejawa na mshangao.

Wamesema familia ya wawili hao haikudhani Syed Rizwan Farook, 28, na mkewe Tashfeen Malik, 27, wangeweza kutekeleza shambulio kama hilo.

Wawili hao waliuawa wakati wa ufyatulianaji wa risasi kati yao na polisi.

Dadake Syed Rizwan Farook, Saira Khan, ameambia CBS News: "Siwezi kufikiria kakangu au wifi wangu akifanya haya, ikizingatiwa kwamba waliokuwa wameoana na walikuwa na furaha nyumbani, walikuwa na binti mdogo wa umri wa miezi sita."

Idara ya uchunguzi wa jinai Marekani FBI imesema inachunguza shambulio hilo la Jumatano kama kisa cha ugaidi.

Hata hivyo, imesema hakuna dalili zozote za kuonyesha wawili hao walikuwa sehemu ya mtandao mkubwa wa kigaidi.

Mkurugenzi wa FBI James Comey alisema mapema Ijumaa kwamba kufikia sasa ushahidi ambao wamepata bado “haueleweki”.

Polisi wanachunguza simu mbili zilizoharibika sana ambazo zilipatikana karibu na nyumba walimokuwa wakiishi wawili hao.

Haki miliki ya picha Getty

Ibada ya kuwakumbuka waliofariki wakati wa shambulio hilo ilifanyika Ijumaa.