Kosa la upigaji chapa la $500m Nigeria

MTN Haki miliki ya picha Getty
Image caption MTN ilipigwa faini kwa kutofungia huduma wateja ambao hawakuwa wamejisajili

Mamlaka inayosimamia mawasiliano Nigeria imesema ilifanya kosa la $500m (£330m) katika upigaji chapa ilipokuwa ikitangaza kupunguzwa kwa faini iliyotozwa kampuni ya MTN.

Tume ya Mawasiliano ya Nigeria (NCC) awali ilikuwa imesema faini ya $5.2bn iliyotozwa kampuni hiyo kubwa zaidi ya mawasiliano ya simu Afrika ilikuwa imepunguzwa hadi $3.4bn.

Lakini msemaji wa NCC Tony Ojobo anasema faini sahihi ni $3.9bn (£2.5bn).

Kampuni hiyo ilipigwa faini Oktoba kwa kukosa kuwafungia huduma wateja ambao hawakuwa wamesajili laini zao za simu.

Kampuni hiyo bado haijazungumzia matukio hayo ya hivi karibuni.

Tangu kutozwa faini mara ya kwanza, kampuni hiyo ya Afrika Kusini ilifanya mabadiliko kadha katika usimamizi wake, huku afisa mkuu mtendaji wake Sifiso Dabengwa akijiuzulu.

Faini hiyo ilipunguzwa baada ya MTN kulalamikia NCC.

“Kulikuwa na kosa. Faini ilifaa kupunguzwa kwa 25%,” Bw Ojobo aliambia shirika la habari la Bloomberg.

"Tuligundua kosa hilo na inabidi turekebishe.”

Kampuni hiyo imetakiwa kulipa faini hiyo kufikia Desemba 31.

MTN ina wateja 231 milioni katika nchi 22 Afrika, Asia na Mashariki ya Kati. Soko lake kuu hata hivyo ni Nigeria.