Uingereza yashambulia tena IS nchini Syria

Ndege Haki miliki ya picha PA
Image caption Ndege za kivita aina ya Typhoon zimetumiwa mara ya kwanza

Ndege za kivita za Uingereza zimeshambulia kwa mara ya pili ngome za wapiganaji wa Islamic State nchini Syria tangu kuidhinishwa kwa operesheni hiyo.

Wabunge waliidhinisha mashambulio hayo Jumatano na muda mfupi baadaye ndege za jeshi la angani la nchini hiyo zikaangusha mabomu kwenye ngome za kundi hilo.

Ripoti zinasema ndege hizo kwa mara nyingine zimeshambulia visima vya mafuta, na kwamba ndege mbili aina ya Tornado zimeshiriki, na kwa mara ya kwanza, ndege mbili aina ya Typhoon. Mapema Alhamisi, ndege nne aina ya Tornado ziliangusha mabomu katika visima vya mafuta vya Omar mashariki mwa Syria.

Ndege hizo zinatumia kambi ya RAF iliyoko Akrotiri nchini Cyprus.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kwenye mashambulio ya kwanza, Uingereza ilitumia ndege aina ya Tornado pekee

Ijumaa, Bunge la Ujerumani nalo liliidhinisha kutolewa kwa usaidizi wa kijeshi kwa vikosi vinavyopambana na wapiganaji hao nchini Syria.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Meli ya kivita ya Sachsen, inayomilikiwa na Ujerumani, itatumwa kusaidiana na meli ya Charles de Gaulle ya Ufaransa eneo hilo

Juhudi za mataifa ya Magharibi dhidi ya kundi hilo zimezidishwa tangu kuuawa kwa watu 127 kwenye mashambulio kadha mjini Paris mwezi uliopita.