Magufuli avunja bodi ya bandari Tanzania

Magufuli Haki miliki ya picha Statehouse Tanzania
Image caption Rais Magufuli amevunja bodi yote inayosimamia bandari

Rais wa Tanzania John Magufuli amevunja bodi simamizi ya bandari siku chache baada ya kupatikana kwa makontena ambayo hayakuwa yamelipiwa ushuru bandari ya Dar es Salaam.

Tangazo la kuvunjwa kwa bodi hiyo limetolewa na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim kwenye kikao na wanahabari. Kampuni 43 ziligunduliwa kuhusika katika makontena hayo.

Prof Joseph Msambichaka ameondolewa kutoka kwa wadhifa wake kama mwenyekiti wa bodi ya bandari sawa na Bw Awadhi Massawe ambaye amekuwa akihudumu kama mkurugenzi mkuu.

Katibu mkuu wa wizara ya uchukuzi Dkt Shaban Mwinjaka pia ameondolewa wadhifani "kuanzia tarehe ya leo na atapangiwa kazi nyingine".

Bw Kassim alifanya ziara ya kushtukiwa wiki iliyopita katika bandari ya Dar es Salaam na ndipo akagundua makontena 329 yalipitishwa bila kulipiwa kodi kinyume na utaratibu wa bandarini.

Waziri huyo mkuu anasema ripoti ya ukaguzi wa ndani iliyotolewa Julai 30 mwaka huu ilionyesha makontena 2,387 yalipitishwa bandarini kinyume cha utaratibu kati ya Machi na Septemba 2014.

"Serikali haitavumilia kuona watu wachache au kikundi chochote kilichojipanga kuhujumu mifumo au kuiibia serikali kwa namna yoyote kwa manufaa ya wachache,” amesema Bw Majaliwa.

Miongoni mwa hatua alizochukua Bw Majaliwa ni kuagiza kubadilishwa kwa mfumo wa malipo hadi mfumo wa kielektroniki ambao unafaa kuwa umekamilika kufikia Ijumaa wiki hii.

Waziri mkuu huyo pia amewasimamisha kazi wasimamizi wanane wa Bandari Kavu.