‘Mfalme wa Wayoruba’ atawazwa Nigeria

Ife
Image caption Ogunwusi ndiye Ife wa 51

Maelfu ya watu walijitokeza kushuhudia kutawazwa kwa mmoja wa wafalme wa Wayoruba ajulikanaye kama Ooni wa Ife.

Mfalme huyo ni mmoja wa wafalme wanaotukuzwa sana kusini magharibi mwa Nigeria.

Adeyeye Enitan Ogunwusi, 40, aliteuliwa Oktoba kumrithi Oba Sijuwade, aliyefariki mwezi Julai akitibiwa jijini London.

Sijuwade alifariki akiwa na umri wa miaka 85.

Wageni wa heshima, akiwemo makamu wa rais wa Nigeria Yemi Osinbajo, walihudhuria sherehe hiyo iliyoandaliwa Ife, katika jimbo la Osun.

Wageni walitumbuizwa na wasakata densi wa kitamaduni chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa usalama.

Ooni wa Ife ni mmoja wa wafalme wenye ushawishi mkubwa zaidi miongoni mwa Wayoruba, ambao ndio wa pili kwa wingi wa watu miongoni mwa makabila ya Nigeria.

Inakadiriwa kwamba kuna Wayoruba 35 milioni wanaoishi Afrika Magharibi.

Ooni wa Ife hutoka kwenye uzao wa Oduduwa, ambaye ni miungu wa Wayoruba. Zamani, Wayoruba walizoea kuzika mtu aliye hai pamoja na mfalme aliyefariki, lakini utamaduni huo ulifutiliwa mbali.