David Miliband alia na waathiriwa wa Boko Haram

Image caption David Miliband

Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Uingereza, David Miliband, amesema kwamba mgogoro wa kibinaadamu ambao unasababishwa na kundi la wapiganaji wa Boko Haram, kaskazini mashariki mwa nchi ya Nigeria haupewi uzito unaostahili na jamii ya kimataifa.

Amesema kwamba watunga sera wa kimataifa na mamlaka za Nigeria wenyewe wanapaswa kufanya juhudi za makusudi kuweza kusaidia waathiriwa wa vurugu hizo za Boko Haram.

Miliband ametoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara katika maeneo ya Kanda ya Kaskazini Mashariki nchini Nigeria.

Milliband ni rais wa kamati ya kimataifa ya uokozi, moja ya vitengo adimu vinavyotoa huduma ya misaada ya kibinaadamu na kusaidia watu waliopoteza makaazi yao kutokana na ghasia.

Katika ziara hiyo, Milliband alikutana na watu waliokimbia makazi yao wakiwemo watoto wenye matatizo kadhaa, wengine ni wanigeria waliolazimika kuwa wakimbizi baada ya kufukuzwa kwa nguvu kutoka nchini Cameroun hivi karibuni.

Bwana Miliband alionyesha wasiwasi wake juu ya kile alichokiita usiri ulioko eneo hilo la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

Inakadiriwa kuwa watu milioni tatu hawana makaazi katika kipindi cha miaka sita ya waasi hao wa Boko Haram ambao wamekwisha ua karibu watu elfu ishirini.

Miliband aliyasema haya alipokuwa akizungumza na mwandishi wa BBC Ishaq Khalid ambaye alikuwa ameandamana naye katika ziara yake.