Nyota wa Hollywood ‘kuhamia Afrika’ Trump akishinda

Jackson Haki miliki ya picha Getty
Image caption Samuel L Jackson ni mmoja wa Wamarekani weusi waliofanikiwa sana Hollywood

Nyota wa Hollywood Samuel L Jackson atahamia Afrika Kusini iwapo Donald Trump atashinda uchaguzi wa urais Marekani, tovuti ya News 24 imeripoti.

Trump, mmoja wa wanaowania tiketi ya kugombea urais Marekani kupitia chama cha Republican, ameshutumiwa vikali baada ya kupendekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani.

Haijabainika iwapo matamshi ya mwigizaji huyo, yaliyopeperushwa kwenye sehemu ya kipindi cha Jimmy Kimmel Live iliyorekodiwa awali Jumatatu, yalitolewa kabla au baada ya matamshi hayo ya majuzi zaidi kutoka kwa Trump.

Bw Trump, wakati mmoja amewahi kunukuliwa akikosoa kundi linalotetea haki za watu weusi Marekani la Black Lives Matter.