Malaysia yatafuta mmiliki wa ndege zilizoachwa uwanjani

Ndege Haki miliki ya picha EPA
Image caption Serikali ya Malaysia imesema imejaribu sana kuwatafuta wamiliki wa ndege hizo

Serikali ya Malaysia imeweka tangazo magazetini ikitafuta mmiliki wa ndege tatu aina ya Boeing 747 ambazo zimeachwa katika uwanja wa ndege Kuala Lumpur.

Tangazo hilo, lililotolewa na mamlaka ya viwanja vya ndege, limeonya mmiliki wa ndege hizo kwamba akikosa kwenda kuzidai katika kipindi cha siku 14 zijazo, basi “tutakuwa na haki ya kuziuza au kuzitumia kwa namba nyingine”.

Mamlaka hiyo imesema ndege hizo pia hazijalipiwa ada ya kutua na ada ya maegesho.

"Hatujui ni kwa nini hawajibu. Kunaweza kuwa na sababu nyingi. Huenda ikawa hawana pesa za kuendelea na shughuli zao,” Zainol Mohd Isa, meneja mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege Malaysia, ameambia shirika la habari la AFP.

Amesema kwa miongo kadha sasa, kuna ndege ambazo zimekuwa zikiachwa uwanjani lakini sana huwa ni ndege ndogo.

Moja iliyoachwa miaka ya 1990 iliuzwa na baadaye ikaanza kutumiwa kama mgahawa katika kitongoji kimoja cha mji wa Kuala Lumpur.

Maafisa wanasema malipo yasipopokelewa kufikia Desemba 21, ndege hizo zitapigwa mnada au ziuzwe zitumiwe kama vyama vikukuu kulipa gharama.