US: Maneno ya Trump ni hatari kwa usalama

Donald Haki miliki ya picha Getty
Image caption Trump amependekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani kwa muda

Wizara ya ulinzi ya Marekani imesema matamshi ya Donald Trump kwamba Waislamu wanafaa kuzuiwa kuingia Marekani ni hatari kwa usalama.

Pentagon imesema matamshi hayo yatasaidia kundi linalojiita Islamic State (IS).

Trump, ambaye anaongoza katika kinyang’anyiro cha kumteua mgombea urais Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, alitoa matamshi hayo baada ya watu 14 kuuawa kwa kupigwa risasi mjini San Bernardino, California.

Afisa wa mawasiliano wa Pentagon Peter Cook amesema matamshi kama hayo yanaendeleza "mtazamo wa Isil”, akirejelea IS.

Pentagon alisema kufungia nje Waislamu kutaathiri sana juhudi za Marekani za kukabiliana na ueneaji wa itikadi kali.

Bila kumtaja Bw Trumo, Bw Cook alisema: “Jambo lolote linaloendeleza mtazamo wa Isil na kuifanya Marekani ionekana kana kwamba inapambana na dini ya Kiislamu ni kinyume na maadili yetu na ni hatari kwa usalama wa taifa.”

Bw Trump ameshutumiwa sana na viongozi mbalimbali duniani tangu atoe matamshi hayo.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry alijiunga na viongozi hao baadaye Jumanne na kusema maneno ya Trump hayasaidii kwa vyovyote katika vita dhidi ya IS.

Wapiganaji wa kundi hilo wamekuwa wakishambuliwa na majeshi ya muungano unaoongozwa na Marekani nchini Syria na Iraq.