Makaburi: Viongozi wa Mandera waachiliwa huru

Viongozi
Image caption Viongozi hao wamehojiwa kwa muda wa saa sita

Viongozi kadha kutoka eneo la Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya, wameachiliwa huru na polisi baada ya kukamatwa kuhusiana na madai ya kuwepo kwa makaburi yaliyozikwa miili ya watu kadha.

Viongozi hao wamehojiwa kwa takriban saa sita.

Seneta Billow Kerrow alikamatwa pamoja na wabunge wengine wanne baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi na kupelekwa makao makuu ya uchunguzi wa jinai.

Jana, Bw Kerrow na wabunge kutoka eneo hilo waliitisha kikao na wanahabari na kuomba msamaha kutokana na madai waliyokuwa wametoa awali.

Walikuwa wamesema kuna makaburi ambayo walikadiria yamezikwa hadi miili 12. Lakini baada ya kufukuliwa, ni mwili wa mwanamke mmoja pekee uliopatikana.

Image caption Ni mwili mmoja pekee uliopatikana baada ya ufukuzi

Waziri wa usalama Kenya Joseph Nkaissery jana alisema waliotoa madai hayo watachukuliwa hatua.