Trump: Sitaacha kuwania urais Marekani

Trump Haki miliki ya picha AP
Image caption Awali Trump ametishia kuwania kama mgombea huru asipotendewa haki chama cha Republican

Mgombea urais Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican Donald Trump amesema hatajiondoa kutoka kwenye kinyang’anyiro cha urais licha ya kushutumiwa vikali kwa matamshi yake kuhusu Waislamu.

BwTrump ameambia gazeti la Washington Post kwamba hatajiondoa, kwa vyovyote vile.

Ikulu ya White House imesema Bw Trump “hajahitimu” kuwania baada yake kusema Waislamu wanafaa kuzuiwa kuingia Marekani.

Alitoa matamshi hayo baada ya wanandoa wawili Waislamu kufyatua risasi na kuwaua watu 14 mjini San Bernardino, California.

Bw Trump ameshutumiwa vikali na viongozi mbalimbali dunia kwa matamshi hayo.

Kiongozi wa karibuni zaidi kumshutumu ni Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, aliyesema Israel "inaheshimu dini zote”, saa chache baada ya Bw Trump kutangaza kwamba atazuru taifa hilo mwezi ujao.

Bw Trump anaongoza miongoni mwa wagombea wanaotaka kuwania urais kupitia chama cha Republican, wiki sita kabla ya vikao vya vyama kuteua wagombea kuanza.

Bw Trump pia amegusia kuwa huenda akawania kama mgombea huru, akiandika kwenye Twitter kuhusu kura ya maoni ya USA Today ambayo imeonyesha 68% ya wafuasi wake wangempigia kura hata kama angeondoka chama cha Republican.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Trump ameshutumiwa vikali kwa kupendekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani

Wasiwasi kwamba huenda Bw Trump akawania kama mgombea huru umewafanya viongozi wa Republican kumsihi mfanyabiashara huyo tajiri kutoka New York aahidi kumuunga mkono mgombea atakayeteuliwa mwishowe.

Hata hivyo, Bw Trump ametishia kuhama chama hicho asipotendewa haki.

“Maisha yangu yote yamekuwa kuhusu kushinda. Huwa sishindwi sana. Huwa nadra sana kwangu kushindwa,” aliambia gazeti la Post.

Viongozi wa Republican wanaogopa kwamba ikifanyika Trump awanie kama mgombea huru, basi atagawanya kura za wafuasi wa Republican na kuwawezesha Democrats kushinda.