Misri: Hakuna ushahidi ndege ya Urusi ilidunguliwa

Image caption Misri 'Hakuna ushahidi ndege ya Urusi ilidunguliwa'

Maafisa wa upelelezi wa ajali za ndege kutoka Misri wamesema kuwa hawajapata ushahidi wowote kuwa ndege ya Urusi iliyoanguka katika rasi ya Sinai na kuua watu 224 ililipuliwa.

Ndege hiyo iliyokuwa ikitokea Sharm el-Sheikh ikielekea Moscow ilianguka jangwani mwezi Oktoba.

Kundi moja la wapiganaji wanaoiunga mkono kundi la Islamic State (IS) walidai kuwa wao ndio walioidungua ndege hiyo.

Takriban watu wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo walikuwa ni raia wa Urusi.

Urusi yenyewe ilitangaza kuwa bomu iliyokuwa imetegwa ndani ya ndege hiyo ya Metrojet Airbus ndiyo iliyosababisha ajali hiyo.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na shirika la Urusi la kusimamia usafiri na ajali za ndege ulipata chembechembe na mabaki ya bomu kwenye eneo la tukio.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Takriban watu wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo walikuwa ni raia wa Urusi.

Urusi iliapa kuwaadhibu waliotekeleza shambulizi hilo.

Hata hivyo kiongozi wa wachunguzi kutoka Misri Ayman al-Muqaddim,amenukuliwa na vyombo vya habari nchini humo akisema kuwa ''Hakukuwa na ushahidi wowote wa kuwepo kwa bomu ndani ya ndege hiyo wala dalili za kitu chochote kilichoathiri usalama wa ndege hiyo.''

Wapiganaji wanaoiunga mkono Islamic State walisema waliiangusha ndege hiyo ilikulipiza kisasi cha mashambulizi ya ndege za Urusi nchini Syria.