Mshukiwa akamatwa kuhusu mauaji ya Paris

Paris Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu 130 waliuawa kwenye mashambulio ya Paris Novemba 13

Polisi nchini Ufaransa wamemkamata mwanamume eneo la Paris kwenye uchunguzi wao kuhusu mashambulio ya Novemba 13.

Polisi wamefanya misako 2,700 tangu kutokea kwa mashambulio hayo, na watu 360 wamewekwa kwenye vizuizi vya nyumbani maeneo mbalimbali Ufaransa, shirika la habari la AFP limeripoti.

Mwanamume wa umri wa miaka 29 aliyekamatwa leo alikuwa akipanga kusafiri Syria, kwa mujibu wa ripoti ya chumba kimoja cha habari Ufaransa.

Polisi pia wamewakamata watu wawili kaskazini mwa Ufaransa na wanazuiliwa na polisi na wakiendelea kuhojiwa.

Afisi ya kiongozi wa mashtaka Paris imesema wawili hao wanashukiwa kumpa bunduki Amedy Coulibaly, aliyeshambulia duka la jumla Januari.

Coulibaly aliua watu wane kwenye duka hilo la jumla, na afisa wa polisi katika kisa tofauti, kabla ya kuuawa kwenye ufyatulianaji risasi na polisi.