Trump yuko buheri wa afya, daktari asema

Trump Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Trump ndiye anayeongoza kinyang'anyiro cha kusaka tiketi ya chama cha Republican

Daktari wa mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump amesema mfanyabiashara huyo mashuhuri yuko buheri wa afya na hana matatizo yoyote makubwa ya kiafya.

Bw Trump amekabiliwa na shinikizo za kumtaka atoe maelezo kuhusu afya yake, kwa kuwa wagombea wengine tayari wamefanya hivyo.

Trump, mwenye umri wa miaka 69 kwa sasa, atakuwa rais mzee zaidi kuchaguliwa Marekani iwapo atashinda urais.

Hata hivyo, daktari wake amesema atakuwa “mtu mwenye afya njema zaidi kuwahi kuwa rais”.

Daktari Harold Bornstein anayehudumu kutoka New York amesema Trump ana nguvu “ajabu” mwilini.

Amepakia kwenye Twitter ripoti ya matibabu ya Trump ambayo alikuwa ameahidi kuitoa wiki kadha zilizopita.

Wagombea waliotoa taarifa zao za matibabu ni pamoja na anayeongoza kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia chama cha Democratic Hillary Clinton na mpinzani wa Trump chama cha Republican Jeb Bush.

"Nina bahati kwamba nilibarikiwa na chembechembe nzuri za kijenetiki,” Bw Trump ameandika kwenye Facebook. “Watu wameshangazwa sana na nguvu zangu, lakini kwangu imekuwa rahisi kwa sababu nafanya jambo nlipendalo.”

Bw Bornstein anasema amekuwa daktari wa Bw Trump tangu 1980, na kwa miaka 39 sasa kiongozi huyo hajakuwa na matatizo yoyote makubwa ya kiafya.