UN yaandaa mazungumzo ya amani ya Yemen

Haki miliki ya picha AFP
Image caption UN yaanda mazungumzo ya amani ya Yemen

Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia unaopigana vita nchini Yemen unasema kuwa usitishwaji mapigano wa siku saba na waasi wa kishia wa Houthi umeanza kutekelezwa.

Usitishwaji huo unaenda sambamba na kuanza kwa mazungumzo ya amani yanayofadhiliwa na umoja wa mataifa yanayofanyika nchini Uswisi.

Mapigano yaliendela hadi dakika za mwisho za kuanza kwa usitishwaji huo huku vikosi vya serikali vinavyosaidiwa na mashambulizi ya angani ya Saudi Arabia vikiteka kisiwa kilichokuwa kikishikiliwa na waasi katika bahari ya shamu.

Watu 6000 wanaaminika kuuawa tangu Saudia Arabia iingilie kati mzozo nchini Yemen mwezi Machi.

Umoja wa mataifa umeiambia pande zote katika mazungumzo hayo kuwa mpango wa kuleta amani huhitaji ujasiri.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Usitishwaji wa mapigano Yemen umeanza sambamba na mazungumzo ya amani yanayofadhiliwa na Umoja wa mataifa nchini Uswisi.

Agenda ya mkutano huo hata hivyo huenda ikawa ngumu kutekeleza.

Dhamira kuu ni kuhakikisha kuwepo kwa usitishwaji wa mapigano kabisa baada ya mkataba wa awali wa kusimamisha vita kwa muda kumalizika.

Aidha mpango wa kuondoa makundi yaliyojihami na silaha nzito nzito, kuruhusu mashirika ya kutoa misaada ya kibinadam katika maeneo yote na pia mpango wa kubadilishana wafungwa ni baadhi tu ya mambo yanayotarajia kujadiliwa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Watu 6000 wanaaminika kuuawa tangu Saudia Arabia iingilie kati mzozo nchini Yemen mwezi Machi.

Hata hivyo masuala hayo yote hayawezi kujadiliwa na kuidhinishwa kwa siku moja au mbili, lakini mabalozi hao wa umoja wa mataifa wanasema watachukua muda unaohitajika.

Haya yote yameashiria jinsi umoja wa mataifa umejitolea kuhakikisha kupatikana kwa mkataba.

Huku asilimia 8o % ya raia wakihitaji misaada ya kibinadam, Yemen haina lingine kwa sasa ila kupatikana na amani.