Utafiti: Wanawake wavutaji sigara huacha kuzaa mapema

Haki miliki ya picha Thinkstock

Wanawake wanaovuta sigara au kukaa na wavutaji sigara wamo katika hatari ya kukatisha uzazi wao mapema, utafiti mpya unaonyesha.

Ripoti ya utafiti ulioshirikisha wanawake 79,000 inasema wanawake waliovuta sigara kuanzia wakiwa na umri wa miaka 15 walikatisha uwezo wao wa kuzaa miezi 21 mapema wakilinganishwa na wale ambao hawakuvuta sigara.

Utafiti huo pia ulionyesha wale ambao wanaishi na watu wanaovuta sigara pia huathirika.

Wataalamu wanasema utafiti huo unaongeza ushahidi kwamba tumbaku ni hatari kwa afya ya binadamu.

Matokeo ya utafiti huo, yamechapishwa katika jarida la kimatibabu la Tobacco Control.

Baada ya kulinganisha wanawake ambao hawajawahi kuvuta sigara na wale wanaovuta sigara sana (zaidi ya sigara 25), walikatisha uzazi miezi 18 mapema.

Na wale waliokaa sana na wavutaji sigara, pia walikatisha uzazi mapema wakilishanishwa na wale wasiokaa karibu na wavutaji sigara.

Watafiti wanasema sumu katika tumbaku huenda zikawa zinavuruga homoni muhimu za uzazi, pamoja na homoni ya oestrogen.