Wafungwa wa Malawi kushindania tuzo kuu duniani

Malawi Haki miliki ya picha Zomba Prison Project
Image caption Nyimbo nyingi kwenye albamu hiyo zimeimbwa kwa lugha ya Chichewa

Bendi moja ya wafungwa kutoka Malawi imefanikiwa kuteuliwa kushindania tuzo kuu za muziki duniani za Grammy.

Bendi hiyo kwa jina Zomba Prison Band imechomoa albamu kwa jina I Have No Everything Here (Sina chochote hapa).

Wengi wa wanachama wa bendi hiyo, yenye wanachama 16 ambao ndio walitunga na kuimba nyimbo kwenye albamu hiyo, wanatumikia vifungo vya maisha jela kwa makosa ya mauaji na wizi.

Washindi wa tuzo za Grammy watatangazwa Februari mwakani, na bendi hiyo itashindania kitengo cha albamu bora zaidi duniani.

Hii ni mara ya kwanza kwa mwanamuziki au kundi la wanamuziki kutoka Malawi kuteuliwa kushindania tuzo hizo.

Wafungwa hao watashindana na vigogo wa muziki kama vile Ladysmith Black Mambazo na Angelique Kidjo.

Ian Brennan ndiye aliyewasaidia kurekodi albamu hiyo mwaka 2013.

Anasema kufikia sasa hajafahamu iwapo wamejulishwa kuhusu ufanisi wa albamu hiyo kwani mawasiliano hupitia kwa mkuu wa gereza.

Haijabainika iwapo wataruhusiwa kuondoka gerezani kwenda kuhudhuria sherehe ya kuwatuza washindi.