Desalegn aonya waandamanaji Ethiopia

Oromo Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waoromo wengi wamekuwa wakitoroka Ethiopia

Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn amesema serikali yake itakabiliana vikali na “makundi yanayohujumu amani” baada ya watu kadha kuuawa kwenye maandamano eneo la Oromia.

Serkali inasema watu watano wameuawa kwenye makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama lakini makundi ya upinzani na watetezi wa haki za kibinadamu yanasema idadi ya waliofariki inakaribia 40.

Akihutubu kupitia runinga ya taifa ya Ethiopia, Bw Desalegn amesema umma pia una jukumu la kutekeleza katika kukabiliana na makundi hayo.

Maandamano hayo yaliyoanza wiki iliyopita yaliongozwa na wanafunzi kutoka kabila la Waoromo ambao hawakufurahishwa na mpango wa serikali ya kupanua eneo la mji mkuu wa Addis Ababa hadi maeneo ya Oromia.

Eneo la Oromia ndilo kubwa kati ya majimbo ya Ethiopia na linazingira mji huo mkuu.

Waoromo wanasema hatua ya kupanua mji huo ni njama ya kutwaa ardhi ya kabila hilo.

Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International limetahadharisha kwamba matamshi ya serikali huenda yakapelekea operesheni kubwa ya kuwaandama waandamanaji na watu wanaopinga mpango huo.

Waoromo ambao ni takriban 27 milioni ndio wengi Ethiopia.

"Matamshi kwamba Waoromo hawa wana uhusiano na magaidi yatawatia wasiwasi sana watetezi wa haki kuhusu kuwepo kwa uhuru wa kujieleza,” mkurugenzi wa Amnesty International katika kanda ya Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu Muthoni Wanyeki, amesema.

Aprili mwaka jana, mpango huo ulisababisha maandamano ya wanafunzi yaliyodumu miezi kadha.

Serikali wakati huo ilisema watu 17 walifariki lakini makundi ya watetezi wa haki yanasema waliofariki walikuwa zaidi ya hao.