Mzozo wa wahamiaji kutawala mkutano wa EU

Wahamiaji Haki miliki ya picha AFP
Image caption Merkel amekuwa akitetea sana wahamiaji wanaoingia Ulaya

Ujerumani na mataifa mengine yatashauriana na Uturuki jinsi ya kuwapa makao maelfu ya wakimbizi wa Syria kabla ya mkutano wa mwisho wa mwaka wa viongozi wa mataifa wa Umoja wa Ulaya.

Wale watakaohudhuria wanatarajia kujadiliana pendekezo la kutaka kuwapa watu kutoka Syria walio katika kambi nchini Uturuki makaazi moja kwa moja.

Hata hivyo Chansela wa Ujerumani Angela Merkel, aliyetoa pendekezo hilo, anakabiliana na upinzani mkali kutoka mataifa mengine ya Ulaya.

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya unaopaswa kufanywa Alhamisi unatarajiwa kumulika tatizo la uhamiaji ambalo limegawa wanachama wa Jumuiya hiyo.

Watu wengi wamewasili Ulaya mwaka huu, jambo ambalo limeyafanya mataifa mengine kujenga nyua kwenye mipaka yao ili kuanza kuthibiti mienendo ya wahamiaji hao.

Wakati huohuo mataifa mengine wanachama yameanza kupuuza mapatano ya Schengen, ambayo yanaruhusu raia wa mataifa hayo ya ulaya kutembeleana bila vibali au mtu kupata visa moja ya kutembelea mataifa yote wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Pendekezo hilo mpya litashuhudia mataifa wanachama wa Jumuiya ya Ulaya yakiwakubali wakimbizi wa Syria wanaotoka kambi za Uturuki moja kwa moja chini ya mpango wa kujitolea.

Inatarajiwa kuwa mpango huo utasitisha watu kusafiri mwendo hatari kupitia bahari hadi Ugiriki na pia wanachama wa Jumuiya hiyo kufurahia mpango huo kuliko kupokea idadi ya watu ambayo wamelazimishiwa.

Mwezi uliopita Uturuki na viongozi wa Ulaya walikubaliana kuwa Uturuki itawazuia wahamiaji kuondoka nchini mwao ambapo mataifa ya Ulaya nayo yatalegeza masharti ya kifedha na kisiasa kwa Uturuki.

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya utajadiliana jinsi ya kuunda kikosi cha muungano huo cha kushika doria fuo za mataifa hao na njia za kuthibiti mipaka yake.

Vita dhidi ya ugaidi ni swala ambalo litamulikiwa pia katika mkutano huo kwa kuwa imethibitishwa sasa kuwa wawili kati ya washambulizi waliohusika katika shambulio la Paris Ufaranza walitumia njia inayofuatwa na wahamiaji kufika Ufaransa.

Wahamiaji wengi wanatoroka manyumbani kwao kutokana na ghasia katika mataifa kama vile Syria, Iraq na Afghanistan, wakitafa kufika Ulaya.