Wajumbe wa Libya waafikiana kuhusu serikali

UN Haki miliki ya picha AP
Image caption Mazungumzo hayo yamefanikishwa na Umoja wa Mataifa

Wawakilishi kutoka mabunge hasimu nchini Libya wametia saini mkataba wa kuundwa kwa serikali ya umoja, kufuatia mashauriano nchini Morocco.

Mjumbe wa UN Martin Kobler akihutubia wajumbe kwenye mkutano huo amesema leo ni “siku ya kihistoria kwa Libya”.

“Mchakato huu wa mazungumzo umeonyesha kwamba Walibya wanaweza kutatua tofauti zao za kisiasa kupitia mazungumzo ya Amani,” amesema.

Hata hivyo ametaja changamoto nne ambazo serikali mpya inafaa kushughulikia, ambazo ni: mgogoro wa kibinadamu, mashauriano ya usalama wa kitaifa, kukabiliana na kundi la Islamic State na makundi mengine ya kigaidi na kuangazia Benghazi na maeneo mengine.

Akiandika kwenye Twitter, balozi wa Uingereza nchini Libya amesema mkataba huo umepokelewa kwa shangwe na Walibya mjini Skhirat.

“Hii ni historia. Nimebahatika kuishuhudia,” amesema.

Libya ilitumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi mwaka 2011.